Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mhe. Mabruki Jabu Makame akitoa maelezo kuhusiana na Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka
Na Jaala Makame Haji - ZEC
Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC imetangaza kuwa Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka
utafanyika tarehe 14 Agosti, 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi
hiyo Ndugu Mlenge Khatib Mlenge.
Akitoa
taarifa ya Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka katika Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi
uliofanyika Ukumbi wa Skuli ya Fedha Chwaka Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.
Mabruki Jabu Makame alisema Tume itafanya uteuzi wa Wagombea kwa ajili ya
Uchaguzi huo tarehe 28 Julai, 2021.
Aidha,
Mhe. Mabruki alisema Wagombea watakaoteuliwa na Vyama vyao wataanza kuchukua na
kurejesha fomu za Uteuzi tarehe 21 Julai mpaka 27 Julai,2021 ambapo kampeni
zitaanza tarehe 29 Julai hadi 12 Agosti mwaka huu.
Katika
taarifa yake Mheshimiwa Mabruki Jabu alisisitiza kuwa Uchaguzi huo kwa mujibu
wa Sheria hautakuwa na Upigaji wa Kura ya Mapema na aliwataka Wananchi, vyama vya Siasa, Wapiga Kura na
Wadau wengine wa Uchaguzi kushiriki kuendelea kudumisha Amani wakati wa matayarisho
hadi kukamilika kwa Uchaguzi huo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali watu, Mipango na Uendeshaji Saaduni
Ahmed Khamis alisema Tume imemteua Ndugu Saidi Ramadhan Mgeni Kuwa Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Chwaka akisaidiwa na Ndugu Jaffar Jihad Juma.
Ndugu
Saadun alithibitisha kuwa takriban mambo yote muhimu kwa upande wa maandalizi
ya kazi ya kuendesha Uchaguzi huo yanakwenda vizuri kwa Mujibu wa ratiba ya
utekelezaji iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Ndugu
Saadun aliendelea kusema kuwa, Upigaji Kura wa uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka
utafanyika katika maeneo na vituo vilivyotumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka
2020 ambapo Orodha ya Wapiga Kura itabandikwa katika Vituo hivyo siku saba
kabla ya siku ya Upigaji Kura ili kuwawezesha Wapiga Kura kufahamu mapema vituo
vyao.
Akitoa
ufafanuzi wa Kisheria Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Uchaguzi Khamis Issa
Khamis alisema kuwa, kwa kuwa Tume imekamilisha Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020
na ina taarifa za Wapiga Kura walioshiriki katika Uchaguzi Mkuu huo, Daftari
litakalotumika kwa Uchaguzi Mdogo wa Chwaka litakuwa lile lile lililotumika kwa
Uchaguzi Mkuu.
Ndugu.
Khamis alivitaka vyama vya Siasa kuteua Wagombea wenye sifa za kugombea kwa
Mujibu wa Sheria ili kuepuka kuwekewa Pingamizi wakati wa uteuzi wa Wagombea
Nao
wadau wa Uchaguzi wadi hiyo, waliiomba Tume kuendeleza jitihada zaidi ya kutoa
elimu ya Wapiga Kura kwa Wananchi wa Vijijini ili kila mmoja apate haki yake ya
Msingi kwani wengi wao wanaoishi vijijini hawana utamaduni wa kutumia vyombo
vya habari ikiwemo mitandao ya Kijamii.
Hata
hivyo, waliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwashirikisha Wadau wa
uchaguzi wakati wa kutekeleza majukumu
yao na kuiahidi Tume hiyo kushiriki katika Uchaguzi huo kwa salama na Amani kwa
kufuata maelekezo yatakayotolea na Tume.
Ilielezwa
kuwa, Tume inaendesha Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka baada ya kupokea taarifa
kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa tarehe 25 Machi, 2021 juu
ya kuwepo nafasi wazi ya Kiti cha Udiwani wa Wadi hiyo kufuatia kifo cha
aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo Bwana Mlenge Khatib Mlenge kilichotokea tarehe 19
Machi, 2021.
No comments:
Post a Comment