Habari za Punde

Tanzania na Filand Zajadili Juu ya Uboreshaji wa Hufuma za Kijamii Kupitia Uwezeshaji wa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Na Mwandishi wetu,Dodoma

Serikali ya Finland imedhamiria kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wanawezeshwa katika utekelezaji wa shughuli zao za uboreshaji wa huduma kwa jamii hususani uwezeshwaji wanawake kiuchumi.

 

Hayo yamebainika mkoani hapa wakati wa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu na Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland hapa nchini  Dkt Timo Voipio yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.

 

Katika  mazungumzo hayo Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland hapa nchini  Dkt Timo Voipio amemuhakikishia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu kuwa Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wanawezeshwa ipasavyo ili kuhakikisha huduma za Jamii zinaboreshwa.

 

Dkt. Timo ambaye pamoja na kubainisha mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali ya Finland nchini, alitaja kuwa uboreshaji wa utoaji wa huduma za kijamii ni moja ya vipaumbele vyao na watahakikisha wanashirikiana moja kwa moja na Serikali ya Tanzania ili kuleta mabadiliko yanayoonekana.

 

Aidha Dkt Voipio amepongeza mikakati iliyowekwa na Wizara ya kuwawezesha Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii katika utekelezaji wa majukumu yao kwani wao ndiyo wanahusika moja kwa moja kukutana na kutatua changamoto za wananchi hadi ngazi za chini.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Jingu amesema kuwa Wizara imeweka kipaumbele mkakati wa kuwawezesha Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa kuwawezesha vifaa vya kazi vikiwemo usafiri na vifaa vya kieletroniki ili kuwezesha ufanisi wa majukumu yao.

 

Halikadhalika, Dkt Jingu amewaomba wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kuwezesha Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii ili kuwasaidia kutatuta changamoto za wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

 

Vilevile Dkt. Jingu amesema kuwa Serikali inaendelea kuwawezesha Wanawake kiuchumi kupitia kukopa isiyo na riba inayotolewa katika Halmashauri zote nchini ili kuwainua kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali. 

 

“Serikali imeweka mipango na mikakati mingi ya kuhakikisha wanawake wanawezeshwa lakini kutokana na kutotosheleza kwa rasilimali fedha baadhi ya makundi ya Wanawake yamekuwa hayafikiwi hivyo bado nguvu za wadau zinahitajika katika hili “ alisema Dkt. Jingu

 

Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt Naftali Ng'ondi amesema kuwa Serikali inatumia mbinu mbalimbali katika kuwezesha mikakati iliyowekwa ya kuwainua wanawake kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta zingine za maendeleo ya Jamii kuhusishwa katika utekelezaji wa mikakati hiyo.

 

Dkt Ng'ondi ameongeza kuwa, kuongezeka wa rasilimali Fedha kutasaidia ufanisi wa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii hivyo kuchochea mabadiliko makubwa kwenye utekelezaji wa mikakati ya kuinua wanawake kiuchumi pamoja na nyanja nyingine za Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.