Habari za Punde

Ujenzi wa Mradi wa Daraja la Tanzanite Wafikia Asilimia 83.5

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa daraja jipya la Tanzanite (Salander) jijini Dar es salaam,

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa daraja jipya la Tanzanite (New Selander) jijini Dar es Salaam na kwamba ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi huo ambao umefikia asilimia 83.5.  

 

Amekagua ujenzi wa mradi huo leo (Alhamisi, Juni 17, 2021). Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 na upana wa mita 20.5, litagharimu sh. bilioni 243.75 na unatarajiwa kukamilika Desemba 14, mwaka huu. Kati ya watumishi 970 wanaofanyakazi katika mradi huo, asilimia 92 ni Watanzania.

 

“Nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa mradi huu ambao umefikia katika hatua nzuri za ukamilishwaji wake. Miradi mingi imefikia hatua muhimu za ukamilishwaji na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameona dalili ya ukamilishwaji ipo na ndiyo maana ameanzisha miradi mingine,”

 

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ushiriki wa Watanzania katika ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini kwa kuwa inachangia katika kuongeza wataalamu. “Watanzania hakuna kinachotushinda, muhimu tuwe na kanzi data ya wahandisi wanaoshiriki katika wa miradi.”

 

Amesema Watanzania wanaofanyakazi katika mradi huo wahakikishe wanafanyakazi kwa umakini ili mradi utakapokamilika waweze kuwa na uwezo wa kujenga wenyewe daraja kama hilo. “Tuhakikishe kila mmoja anakuwa mahiri katika fani yake kama ni kuchanganya zege au kusuka nondo.”

 

Ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na kampuni ya GS Engineering Corporation kutoka Korea Kusini una lengo la kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambayo inatumiwa na magari mengi yanayoingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.

 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi wa ujenzi wa daraja hilo kwa sasa upo katika hatua za ukamilishwaji wa eneo la juu na tayari mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 175.4.

 

 IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, JUNI 17, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.