Habari za Punde

Juhudi Zinahitajika Kuendeleza Vipaji vya Wabunifu wa Sinema Zanzibar.

Na. Maulid Yussuf WEMA ZANZIBAR

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema  bado  juhudi zinahitajika ili kuendeleza vipaji vya wabunifu wa sinema mbalimbali nchini.

Amesema hayo Kwa niaba ya Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mhe Tabia Maulid Mwita, wakati wa hafla ya usiku wa zawadi wa Tamasha la Kimataifa la filamu Zanzibar, (Zanzibar International Film Festival)  katika ukumbi wa Ngome kongwe Unguja.

Amesema kuboresha tamasha hilo kutasaidia sana kuibua vipaji vya Vijana na kuitangaza Zanzibar kiutalii zaidi pamoja na kupelekea jina la Tanzania liendelee kukua nchi za Nje.

Aidha mhe Simai  amesema akiwa mwenye dhamana ya elimu nchini ata hakikisha anainua vipaji  katika Skuli mbalimbali ili kukuza tamasha hilo kwa kuwa na wabunifu wazalendo.

Mapema Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF  bwana Hassan Mitawi amesema tamasha hilo linaleta  muamko kwa Wazanzibari  katika suala la utunzaji mazingira bila ya kuharibu mila zao.

Amesema tamasha hilo linawakilisha maonesho mbalimbali ambayo yanaelimisha na kuihamasisha jamii juu ya kujilinda na maradhi, kulinda mazingira  na kudumisha mila na tamaduni za Kizanzibari hali inayopelekea  Zanzibar kuzidi kujulikana duniani kote na kuwa  kivutio kikubwa cha utalii.

Nae  CEO bwana Martin Muhando amesema tamasha  la ZIFF linawasilisha utamaduni wa Zanzibar pamoja na wakaazi wake hasa katika masuala ya utamaduni wao ambapo huwavutia sana wageni wanaokuja kutembelea visiwa vya Zanzibar.

Amesema kutokana na mazingira mazuri na ukarimu  wa watu wa  Zanzibar   imepelekea kuwa na ongezeko la  wadhamini na wadau wengi ambapo pia linaongeza furaha na amani  kwa wageni na wenyeji wa visiwa vya  Zanzibar.

Aidha wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kulisimamia  tamasha la Zanzibar International Film Festival kuendelea kubaki Zanzibar kwani ndio asili ya Tamasha hilo.

Tamasha la 24 la ZIFF limeshirikisha jumla ya filamu 67, ikiwa filamu 11 kati ya hizo zimeonekana kufanya vizuri kwa mwaka huu,  ambapo filamu ya RUPIA imeshinda tunzo ya EMARSON kwa mwaka 2021.

Hafla ya Usiku wa zawadi ni miongoni mwa shamrashamra za 24 za tamasha la Zanzibar International Film Festival ambazo hufanyika kila mwaka visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.