Wadau
/ wanaharakati watetezi wa haki za Wanawake, Vijana na Watoto wamependekeza
Tume ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ishirikishe wajumbe wengine kutoka sekta mbali mbali zikiwamo
asasi za kiraia ili kuangalia, kujadili, kushauri na kupendekeza utendaji mzuri
wa usimamizi wa mchakato mzima wa uchaguzi na mwenendo wa vyama vya siasa.
Maamuzi
hayo yamekuja baada ya kufanya utafiti mdogo wa kupitia Sera ya Jinsia na
Ujumiushi (Gender and Social Inclusion Policy) ya (ZEC) ya mwaka 2015 na kuona mapungufu yaliyosabisha wanawake, vijana
na watu wenye ulemavu kutoshiriki ipasavyo katika mchakato wa chaguzi
zilizopita.
Wadau hao ni pamoja na Mtandao wa Jinsia Zanzibar (ZGC), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya inayojihusisha na Kupambana na Changamoto zinazowakabili Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Jumuiya ya Vijana Zanzibar (ZYF) na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) ambapo walibaini mapungufu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na mwongozo na mpango mkakati wa kuitekeleza sera ya jinsia na ujumuishi ambayo imeundwa maalum kwa ajili ya kuangalia ujumuishi na haki za kijinsia, vijana na watu wenye ulemavu zinazingatiwa katika mchakato mzima wa uchaguzi ili demokrasia siyo tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka.
.
Hivyo wamependekeza kuwe na mwongozo maalum katika kila hatua ya uchaguzi kuanzia uandikishaji, utoaji wa elimu ya uraia, uteuzi wa wagombea, usimamizi wa uchaguzi, upigaji kura, utoaji wa matokeo na hali ya usalama na kwamba suala la usawa wa kijinsia na ujumuishi liongoze mchakato wote wa uchaguzi kabla, wakati na baada.
Wadau pia wamependekeza kuwa ili kuhakikisha usawa wa kijisia na ujumuishi unafikiwa kwa kila ya hatua ya uchaguzi ZEC inapaswa kukutana na wadau wa masuala ya jinsia, vijana na watu wenye ulemavu mara kwa mara ili kuona hali ikoje na kuweka mpango wa utekelezaji ili pia kusaidia katika ukusanyaji wa takwimu kama sera ilivyosema kuwa ZEC itakuwa na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa takwimu (Systematically Data Collection).
Mwenyekiti wa JUWAUZA Bi
Salma Saadat amesema pia katika utafiti wamebaini uwepo wa kamati ya maadili
ya ZEC
ni wa muda mfupi, huundwa wakati wa uchaguzi na uhai wake humalizika mara tu baada ya
uchaguzi kwisha.
Pia kamati hiyo
haijawekewa mwongozo wa kushughulikia malalamiko wala
haina mwongozo wa kutatua vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu wakati wa uchaguzi.
“Kuna
wanawake walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wakati wa uchaguzi lakini
hawajui waende wapi kupeleka kesi zao, kwa sababu kamati haina mwongozo wa
kutatua kesi za mtu mmoja mmoja, kamati inapokea kesi za vyama vya siasa tu kwa
mfano kesi ya ACT Wazalendo kuhusu kiongozi wao kupinga kuwapo kwa kura za
mapema ambapo alituhumiwa kuvuruga amani,” alisema Bi Salma.
Hivyo wamependekeza sera hiyo iweke mwongozo na mpango kazi ili ikidhi haja kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika mchakato mzima wa uchaguzi kama wapiga kura, wagombea, wafuatiliaji ilani na sera za vyama na hata kuhakikisha kuwa usalama wao unalindwa vyema.
Aidha
Wadau wamependekeza Sera ya Jinsia na Ujumishi ya ZEC ipitiwe tena pamoja na
kuipangia mpango kazi ili iweze kutekelezeka, wamesema ni vizuri ikawepo kamati
ya maadili ambayo ni shirikishi inayozingatia uwiano wa kijinsia na ujumuishi
wa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Vile
vile katika mapendekezo wadau wameomba
katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
ifanyiwe marekebisho ili wanawake waweze kuteuliwa kwenye nafasi ya Makamishna
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa sababu katiba iliyopo sasa haimlazimishi Rais
wa Zanzibar kuzingatia usawa wa jinsia wakati wa kuteua Makamishna wa Tume ambapo kwa sasa ZEC ina kamishna mmoja
tu mwanamke na sita ni wanaume ikiwa ni sawa na asilimia 14 tu.
“Tunafahamu
kuwa mamlaka ya uteuzi wa makamishna siyo wa ZEC kwa kuwa imeainishwa katika Katiba
ya nchi kwamba mwenyekiti na wajumbe wengine wawili watateuliwa na rais, ambapo
kati ya hao lazima mmoja awe jaji na wajumbe wengine wanne watatoka katika
vyama vya siasa.
“Ili
kuhakikisha kwamba ZEC inasimamia vyema Sera yake ya Jinsia na Ujumuishi
ilisema kwamba mara kwa mara itakua inapendekeza kufanya marekebisho ya katiba
ili masuala ya jinsia na ujumuishi yaingie katika katiba na kuifanya sera hii
itekelezeke, hivyo tunashauri hatua hiyo ifanywe mapema iwezekanavyo kabla ya
uchaguzi mkuu mwingine kwa sababu kumalizika kwa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi
mwingine,” alisisitiza Bi Salma.
Dkt. Mzuri Issa
Mkurugenzi,
TAMWA, ZNZ
No comments:
Post a Comment