RAYA HAMAD – OMKR
MKOA WA MJINI
MAGHARIBI
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya
yanahitaji nguvu ya pamoja ili kuhakikisha nchi inashinda vita hio na jamii haina budi kuongeza kasi ya kushirikiana
katika kupambana na janga hili na kuwaokoa walioathirika.
Waziri wa nchi
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saaada Mkuya Salum ameyasema hayo
katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi mipango sera na utafiti Bi
Daima Mohamed Mkalimoto wakati akiyafunga mafunzo ya huduma masafa kwenye
ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani
Dkt Saada amesema matatizo yanayofanywa na
watumiaji wa dawa za kulevya katika jamii yasipelekee kuwakataa na kuwatenga,
kwani wao bado ni sehemu ya jamii yetu
‘Tuendelee kuwafikia
zaidi na kuwapatia taaluma juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya pamoja
na kuwapa ushauri nasaha, kwa namna hii sisi tutakuwa chanzo cha kuwaepusha na
msongo wa mawazo, naomba kutoa wito kwetu sote tusimame pamoja katika kuiokoa jamii yetu”
alisisitiza Dkt Saada
Aidha amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, inaendelea kuchukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto ya matumizi,
uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya na madhara yanayotokana na
matumizi ya dawa za kulevya.
Kumbukumbu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa
kuna takriban watumiaji wa dawa za kulevya 10,000 kati yao watu 3,200 wanatumia
dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, hali inayohatarisha maisha yao na jamii
inayowazunguka
Dkt Saada ametoa shukrani kwa Jumuiya ya
waliopata nafuu (Recovery Community) kwa uamuzi wao wa kuandaa mafunzo hayo
yenye lengo la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya.
Kuwafikia walioathirika
wa dawa za kulevya na kuwapatia huduma stahiki ambazo zitawasaidia kujiokoa na
jinamizi la utumiaji wa dawa za kulevya jambo ambalo linadhihirisha ushiriki wao
kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Mkurugenzi wa huduma
masafa ndugu Abdulrahman Abdallah Mani
aliyepata huduma nafuu kutoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya na mmoja kati
ya waandaaji wa mafunzo hayo amesema kuwa wanampango wa kuanzisha
kituo kijulikanacho kama Drop in Centre
Kituo hicho kitawakusanya
vijana mara baada ya kutoka katika nyumba za upataji nafuu na kuwasaidia
shughuli za kufanya na kujiendeleza ili kuepuka vishawishi vya kurudia tena
matumizi ya dawa za kulevya.
Mani amesema kituo
kitasaidia kutoa fursa mbali mbali kwa walioathirika wa dawa za kulevya na
huduma rafiki ikiwemo elimu, ushauri
nasaha kwani wengine hujiingiza pasina kufahamu athari ya janga hili
Nae mkufunzi wa mafunzo hayo Bwana Abdalla Badrus
kutoka Mombasa Kenya amesema kuwa taaluma iliyotolewa katika kuwafuatilia
vijana walioko kwenye mazingira magumu ya matumizi ya dawa za kulevya hapa
Zanzibar itasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kuijenga Afrika ya Mashariki
isiyo na matumizi ya dawa za kulevya
Badrus amesema iwapo washariki hao watajitahidi
kuandika na kuomba miradi kwa kutumia elimu aliyowapatia na mtiririko wa
kiuandishi wenye kufuata vigezo hakuna shaka kituo cha Drop in center kitakuwa
endelevu na huduma itawafikia vyema walengwa
“hakikisheni mnajituma na kuwa wabunifu
mkiandika vizuri wahisani watawaitika misaada itawafikia na mtaweza kutoa
huduma kwa kuwafikia vijana walio wengi ambao ndio waathirika wakuu wa matumizi
ya dawa za kulevya” alisisitiza Badrus
Mafunzo hayo ya
siku 4 yameandaliwa na Jumuiya ya waliopata nafuu (Recovery Community) ambapo
washiriki 50 kutoka taasisi za Serikali na Binafsi wameshiriki wakiwemo Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya,
Maafisa wa Chuo cha Mafunzo, Vijana waliopata nafuu na baadhi ya asasi za
kiraiya
No comments:
Post a Comment