Habari za Punde

Mhe Hemed akerwa na uchafu wa barabara, mitaro na suala la usafi

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwagiza viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Mjini kuchukua hatua za haraka katika kutatua changamoto ya Mitaro ya maji Machafu wakati alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais akiambatana na viongozi  wa serikali akitembelea maeneo mbali mbali ya jiji la Zanzibar akiwa katika ziara maalum ya kukagua haiba ya Jiji hilo.
Mhe. Hemed akitoa maelezo katika majumuisho kupitia ziara yake alioifanya ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar ambapo amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Uongozi wa Kituo cha Afya cha Rahaleo.

Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba Maendeleo na Makaazi na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kukaa pamoja kwa lengo la kuzitatua changamoto mbali mbali ndani ya Jiji la Zanzibar.

Mhe. Hemed alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara katika maeneo yanayozunguka nyumba za wananchi Michezani mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema hajaridhishwa na muonekano wa maeneo hayo kutokana na hali mbaya akitolea mfano juu ya muonekano mbaya wa barabara, mitaro na suala la usafi katika maeneo hayo.

Alisema kuwepo kwa mitaro mibovu katika njia hizo inahatarisha usalama wa wananchi na Afya za watoto wanaocheza na kupita katika mazingira hayo.

Akigusia suala la maji safi na salama Mhe hemed aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeweka mkakati madhubuti wa kuwapatia huduma hiyo wananchi wake kwa muda wote bila ya udhia wowote.

Kuhusu wananchi wanaokaa katika nyumba za wananchi Michezani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar kuhakikisha nyumba hizo wanapewa wananchi wanaostahiki bila ya upendeleo.

Alieleza azma ya muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kujenga nyumba hizo ni kuwapa makazi bora wananchi wanyonge wa Zanzibar.

Akijibu malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kuhusiana na upigaji wa miziki kwa sauti ya juu majumbani, Mhe. Hemed aliwaagiza Masheha kukaa pamoja na Mkuu wa wilaya kuweka utaratibu mzuri utakaoridhiwa na wengi ili kuhakikisha wananchi hawabuguziwi na kadhia hiyo.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed alikasirishwa na tabia ya wananchi kuvunja sehemu ya jumba namba kumi na kulitumia eneo hilo lisilo rasmi kwa matumizi ya utupaji wa taka.

Aidha, aliuagiza uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji kuchukua hatua ya haraka kutengeneza barabara ya kituo hicho, ili kurahisisha wananchi kuweza kufika kituoni hapo bila ya kikwazo chochote.

Nao wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa mingoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na kukithiri kwa uchafu katika maeneo hayo kunakosababishwa na usimamizi mbaya na watendaji wa baraza la Manispaa.

Aidha, walisema kumekuwepo na tatizo la watu wanaojitokeza kufungua redio majumbani kwa sauti za juu jambo linalosabisha kero kwa wakaazi wa maeneo hayo.

Pamoja na mambo mengine wananchi hao walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kwamba wanasikitishwa na harakati zainazoendeshwa katika maeneo ya viwanja vya Mnazimmoja hali inayosababisha kuharibiwa kwa viwanja hivyo, huku ikisababisha kupotea kwa lengo lililoasisiwa na Muasisi wa Taifa la Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

Wakijibu changamoto za wananchi viongozi walioambatana na Makamu wa Pili wa Rais katika ziara hiyo walisema kumekuwepo kwa tatizo kubwa la kukiukwa taratibu zinazofanywa na wakaazi wa nyumba hizo ikiwemo changamoto ya ulipaji wa kodi, ujenzi usiofuata taratibu unaosababisha kuharibu miundombinu ya kupitishia maji.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziabr alipata fursa ya kutembelea Kituo cha Afya Rahaleo ambapo ameridhishwa na huduma zinazotolewa kituoni hapo.

Akizungumzia Changamoto zinazokikabili kituo Daktari dhamana wa Kituo cha Afya Rahaleo Ashura Miraji Mpatani alisema kituo kinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa eneo pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji kutoka katika laini kuu ya bomba la mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.