Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia)
akitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali katika Mkutano uliofanyika katika
Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Septemba 13, 2021.
Ulega alifanya ziara Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za
Wakulima na Wafugaji ambapo baada ya kusikiliza kero hizo aliagiza kuundwa kwa kamati za maridhiano
zitakzaokuwa zinashughulika migogoro hiyo mapema inapojitokeza.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kuhakikisha wanaunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo na kuleta madhara kwa jamii.
Ulega alitoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Septemba 13, 2021 baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika Wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.
Katika Mkutano huo wananchi wa Kijiji hicho walililalamikia Jeshi la Polisi katika Wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka pale wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Wakulima hao walisema kuwa wafugaji wanaofanya vitendo hivyo
wengi ni wahamiaji katika maeneo hayo na hivyo wamekuwa wakiwasababishia matatizo
makubwa ikiwemo kuharibiwa kwa mazao yao na wanapotaka kufanya jitihada za
kulinda mazao yao wanaishia kupata kipigo.
Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na sehemu kubwa ya
wakulima hao, Waziri Ulega alitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali kuanzia
ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na
migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara.
Aliongeza pia kwa kulitaka Jeshi la Polisi Wilayani humo
kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mtu na kwa usawa ili kuondoka lawama
zinazowakabili za kuonekana wanawapendelea wafugaji kuliko wakulima.
Vilevile, aliwaekeza
watendaji wa wilayani humo kuwa katika kamati hizo watakazoziunda waandae
mpango mzuri wa kuweka njia kwa ajili ya kupitishia mifugo ili isiwe inapita
katika mashamba ya wakulima.
Aidha, Waziri Ulega alitumia ziara hiyo pia kukemea vitendo
vya kujichukulia Sheria mkononi vinavyofanywa na wakulima pamoja na wafugaji
akisema kuwa kufanya hivyo ni kosa na ni miongoni mwa vitendo vinavyochangia
uvunjifu wa amani.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa katika
kuhakikisha maelekezo hayo ya Naibu Waziri yanafanyiwa kazi kwa haraka
aliwaagiza Watendaji wake kuhakikisha kamati hizo zinaundwa ndani ya wiki moja.
kuhusu suala la kuweka njia za mifugo, Kawawa alitoa mwezi
mmoja kwa wataalam mifugo kwa kushirikiana na wafugaji na wakulima kuhakikisha
njia hizo zinawekwa ili kupunguza usumbufu wa mifugo katika mashamba ya
wakulima.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo pia aliwataka wafugaji kuchimba
mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo yao na kwa kufanya hivyo kutasaidia
kupunguza migogoro ya mara kwa mara na
wakulima.
Kabla ya ziara hiyo ya Waziri Ulega Wilayani humo, siku
chache zilizopita wafugaji waliuwawa kutokana na migogoro hiyo hiyo ya wakulima
na wafugaji katika Kijiji cha Nanjilinji.
No comments:
Post a Comment