Habari za Punde

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Kwahani Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, akikata utepe kulifungua Jengo Jipya la Tawi la CCM Sebleni Jimbo la Kwahani na (kushoto kwa Rais) Mbunge wa Jimbo la Kwani Mhe Ahmada Yahya Abdulwakil na (kulia kwa Rais) Katibu wa CCM Jimbo la Kwani Ndg.Ramadhani Juma na Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Kwahani Khamis Yussuf Pele
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi. akiwahutubia Wananchi wa Jimbo la Kwahani Zanzibar, wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la Tawi la CCM Sebleni na Kisiwa cha Maji Safi na Salama Sebleni
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi wa Jimbo la Kwahani kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo wakati alipokuwa akiwahutubia wana CCM pamoja na wananachi mara baada ya kulizindua Tawi la CCM la Sebleni lililojengwa upya pamoja na kuzindua kisima cha maji safi na salama kiliopo katika eneo hilo la Tawi la CCM la Sebleni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika hotuba yake  hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uongozi wa Jimbo hilo umeweza kutekeleza mambo makubwa mawili likiwemo la kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Jimbo lao hilo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari viongozi hao wa Jimbo la Kwahani wameshafanya kazi  nyingi katika kutoa huduma za jamii ikiwemo hatua hiyo ya ujenzi wa kisima cha maji safi na salama kazi ambazo zimefanywa kwa mashirikiano ya pamoja.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa vipindi vitatu kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alieleza mipango ya Serikali ya kuimarisha huduma za jamii ukiwemo mradi mkubwa wa maji safi na salama unaondelea katika Wilaya ya Magharibi ‘A’, Magharibi ‘B’ na Wilaya ya Kati kupitia Benki ya Exim ya India, huku akisisitiza kwamba hatua hiyo itaendelea na kwa Wilaya nyengine zilizobaki.

Rais Dk. Mwinyi  alitumia fursa hiyo kueleza mpango ya Serikali anayoiongoza  ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 220 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ujenzi ambao utafanyika ndani ya miezi 24.

Aliongeza kuwa kwa upande wa sekta ya afya tayari mipango madhubuti imeshapangwa katika kuhakikisha Serikali inaiimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma hatua ambayo pia itachangiwa na fedha zipatazo Dola milioni 100, zilizotolewa kwa ajili ya mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Miwnyi aliwaeleza wanaCCM pamoja na wananchi kwamba hatua za Serikali zinazochukuliwa dhidi ya wizi wa fedha za umma ni juhudi za makusudi katika kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinawafaidisha walio wengi badala ya kuwafaidisha wachache hatua ambayo inafanywa kwa nia njema.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba lengo kubwa ni kuhakikisha utendaji Serikali unaimarika na unakuwa bora.

Nao viongozi wa Jimbo hilo walieleza kwamba wanaridhika na uongozi wa Rais Dk. Miwnyi ambao umeweza kuendeleza amani, umoja, utulivu na mshikamano mkubwa hatua ambayo imeweza kuimarisha maendeleo nchini.

Viongozi hao waliwataka wananchi na WanaCCM wa Jimbo hilo waweke matarajio makubwa kwani mambo mazuri zaidi yanakuja katika Jimbo lao huku wakisisitiza kwamba mafanikio ya Jimbo lao yanatokana na umoja na mashirikiano makubwa yaliopo kati ya viongozi hasa Mbunge na Mwakilishi ambao wamekuwa kitu kimoja katika kuwatumikia wananchi sanjari na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mapema Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mjini Kichama, Tali Ali Talib alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kutokana na juhudi zake za uongozi pamoja na kuwapongeza viongozi wa Jimbo hilo kwa mashirikiano yao katika kuwaletea maendeleo wananchi ikwia ni pamoja na kuwasogeze huduma za kijamii pamoja na kuwajengea Tawi la CCM la aina yake  kwa azma ya  kutekeleza Ilaini  ya Uchaguzi ya CCM.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.