Habari za Punde

Wizara ya Elimu kuendelea kuwekeza sekta ya Elimu

 Na Maulid Yussuf WEMA

ZANZIBAR.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), imesema itaendelea kuwekeza kupitia sekta ya elimu ili kwenda sambamba na malengo ya Serikali juu ya kutoa elimu bila malipo kwa wote.

Waziri wa wizara hiyo Simai Mohammed Said amesema hayo wakati alipofungua maonesho ya kitaaluma ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusheherekea miaka 57 ya elimu bila malipo.

Amesema Wizara ya Elimu itaendelea kuongeza vifaa vya kufundishia katika Skuli zote za Unguja na Pemba ili kuwafanya vijana waweze kujifunza kwa ufanisi na kuleta maendeleo ndani ya nchi yao.

Amefahamisha kuwa Serikali imeweka sera na sheria juu ya suala hilo ili kuona kila mwananchi anapata haki hiyo bila ya ubaguzi.

Amefahamisha kuwa Wizara hiyo itazidi kuwaandaa vijana na kuviendeleza vipaji viliyopo ili kuhakikisha vinauzika katika soko la ajira liliyopo ndani na nje ya nchi ambapo hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa wataalamu wa ndani waliyobobea katika fani mbalimbali.

Akizungumzia suala la maonesho hayo Mhe, Simai amesema yatasaidia kuielimisha jamii katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo pamoja na kujifunza vitu mbalimbali kupitia  maonesho hayo.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba jamii na Wanafunzi kutumia siku tatu hizo katika kupata elimu mbalimbali iliyopo katika maonesho hayo sambamba na kuwaomba  wadau  mbalimbali kuzidi kushirikiana ili kupata maendeleo bora katika sekta ya Elimu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo bw Ali Khamis amesema Serikali itaendelea kutoa elimu bure ili kwenda sambamba na malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni, bi Sichana Haji Foum amesema lengo la maonesho hayo ni kuonesha vipaji na maendeleo mbalimbali yaliyopo katika sekta hiyo.

Amefahamisha kwamba Wizara hiyo inatoa elimu kwa watoto wote hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi wenye watoto walio na mahitaji maalum kuwapeleka Skuli ili waweze kupata haki zao za msingi na kuwekeza katika elimu badala ya kuwaficha majumbani.

Amesema mara nyingi watoto hao huonekana hawana haki ambapo baadhi yao wanawaficha na kukosa haki yao ya msingi, hivyo Wizara hiyo imejipanga kwa kuwa na Skuli na madarasa ya kutosha kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao ili waweze kutambulika katika sehemu mbalimbali.

Maonesho hayo ya siku tatu yameandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibaf,  ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusheherekea miaka 57 ya elimu bila malipo hapa Zanzibar,  ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Matumizi sahihi ya Tehama katika mazingira ya UVIKO 19 yatarahisisha elimu bora nchini’’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.