Habari za Punde

SEKTA YA POSTA NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA UCHUMI - DKT. YONAZI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati akifungua Semina kwa watoa huduma za Posta iliyofanyika Dodoma. 

Sehemu ya washiriki wa semina ya watoa huduma za Posta wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina hiyo iliyofanyika Dodoma.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi ameizungumzia Sekta ya Posta kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla kwasababu inawezesha usafirishaji wa mizigo popote duniani

Hayo ameyazungumza wakati akifungua semina ya watoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na vifurushi nchini wenye leseni ya kufanya huduma hizo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo kujadili maendeleo na maboresho ya Sekta hiyo nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika la Posta Tanzania na wadau wake wanaadhimisha wiki ya Posta duniani ambayo kilele chake ni tarehe 9/10/2021

Dkt. Yonazi amezungumzia mkutano huo kuwa utasaidia kujadili namna ambavyo Serikali inaweza kuendelea kuwekeza na kuboresha huduma za usafirishaji, kuleta ubunifu mpya na huduma mpya na pia kuwa mabalozi wazuri wa Sekta ya Posta na huduma za ugavi ili ziweze kuleta tija kwa maendeleo ya Taifa

Amesema kuwa Serikali imewekeza katika Sekta ya Posta ili kuhakikisha kunakuwa miundombinu rafiki ya usafirishaji na ugavi huku akiitaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ambazo hadi sasa halmashauri 21 nchini tayari zimeshafikiwa na muundombinu huo na mipango inaendelea kwa nchi nzima kufikiwa na muundombinu huo

Ameongeza kuwa mfumo huo unaohusisha majina ya mitaa, barabara na namba za nyumba  itawezesha na kurahisisha uchukuaji na ufikishaji wa mizigo pamoja na ufikishaji wa huduma mbalimbali kama zimamoto na polisi pale zinapohitajika

Aidha, amesema kuwa kwa upande wa postikodi kila kata sasa ina postikodi yake na zinatambulika katika mfumo wa postikodi na mwananchi anaweza kufahamu postikodi yake kwa kupiga *152*00# na kufuata maelekezo ambayo yatampatia namba ya postikodi ya eneo husika na kwa sababu namba hizi zinatofautiana zinarahisisha mhusika kufikiwa pale alipo

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Kuwe amesema Mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na watoa huduma wa Sekta ya Posta angalau mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu Sekta hiyo nchini na kipindi hiki kinawaunganisha pamoja kuelekea maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani

Amesema kuwa katika kipindi hiki cha UVIKO 19, sekta nyingi ziliathiriwa na mlipuko wa UVIKO 19 ambapo kwa upande wa Sekta ya Posta baada ya kujikita na matumizi ya teknolojia imeendelea kuimarika kwa sababu mtu anaweza kuagiza bidhaa mtandaoni na Shirika la Posta likamsafirishia na kumfikishia mpaka mlangoni

Ameongeza kuwa Serikali kupitia TCRA imeruhusu ushindani katika Sekta ya Posta ili kuboresha utoaji wa huduma, ubunifu na kuleta tija kwa taifa katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuyapatia leseni makampuni binafsi yanayofanya huduma za usafirishaji

Naye Afisa Masoko wa DHL, Abdallah Sharrif amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yametoa fursa kubwa kwao kama watoa huduma ya usafirishaji kujumuika na Shirika la Posta Tanzania pamoja na mashirika mengine ya usafirishaji na mawasiliano nchini

Aidha amesema kuwa wao kama watoa huduma kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania wameweza kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wananchi na wafanyabiashara wadogo wadogo wanaohitaji huduma za usafirishaji kwa uharaka ndani ya nchi na nje ya nchi

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.