Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amekutana na kuzungumza na kiongozi mkuu wa Kanisa la Efatha Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Kanisa la Efatha, ukiongozwa Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo.Bw. Josephat Elias Mwingira (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 22-11-2021.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza utayari wa uongozi wa Kanisa la Efatha wa kuunga mkono juhudi za  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha huduma za kijamii.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kanisa la Efatha lenye Makamo Makuu yake Mwenge Jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo Josephat Elias Mwingira uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa  anafarajika kwa kiasi kikubwa pale anapopata watu wa kumuunga mkono katika kuendelza shughuli mbali mbali za maendeleo na kijamii katika kuwahudumikia wananchi.

Alisema kuwan hatua za uongozi wa Kanisa hilo la Efatha zinatoa matumaini makubwa katika kuhakikisha kwamba juhudi anazozifanya zimekuwa zikithaminiwa na kuungwa mkono kwani tokea alipoingia madarakani ameshuhudia makundi kadhaa ya kijamii yakiwemo madhehebu ya kidini yameonesha ushirikiano mkubwa kwake pamoja na serikali anayoiongoza.

Alisema kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika uongozi wake kutokana na wananchi kuwa wamoja na kuweza kuondokana na matabaka katika jamii yakiwemo matabaka ya kidini.

Aliongeza kuwa hatua za Kanisa hilo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu, afya pamoja na ujenzi wa vituo vya Polisi kuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi na kutoa huduma za kijamii.

Alieleza kwamba kwa vile Zanzibar ni nchi ya utalii hatua za ujenzi wa vituo vya Polisi kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha amani na usalama kwa wananchi pamoja na wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa kuamini kwamba nchi iko salama.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba hivi sasa Zanzibar imo katika hatua za makusudi za kufanya mageuzi ya elimu hivyo, hatua za uongozi huo za kuahidi kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwatumia watalamu wake zitasaidia kufikia lengo hilo lililokusudiwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliuahidi uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari na itaendelea kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha azma inapatikana.

Mapema  Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo Josephat Elias Mwingira alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kupata neema ya kuwa Rais wa Zanzibar ambapo ndani ya mwaka mmoja mafanikio makubwa yameweza kupatikana.

Aidha, Mwingira ambaye amefika Ikulu pamoja na uongozi wa Kanisa hilo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi kwa vile ana hofu ya Mungu ameweza kuwaunganisha wananchi wa makundi yote bila ya kujali dini, chama, kabila wala jinsia.

Alieleza kuwa utendaji wa Rais Dk. Mwinyi umeweza kufanikiwa kutokana na kiongozi hyo kutokuwa na ubaguzi wa aina yotote ambapo kwa upande wao wakiwa viongozi wa Kanisa la Efatha, wameridhika na juhudi hizo na kuahidi kumuunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Alifahamisha kuwa, uongozi uliotukuka wa Rais Dk. Mwinyi umepelekea Zanzibar kuwa na umoja ulio imara na kuahidi kwamba uongozi wa Kanisa hilo utaendeleza utamaduni wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya elimu, afya, ujenzi wa vituo vya Polisi pamoja na kuendeleza sekta nyengine za maendeleo.

Pamoja na hayo, Kanisa hilo limeahidi kuendelea kuwatumia wataalamu wake katika kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta ya elimu.   

Imetayarishwa na kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Efatha.Bw. Josephat Elias Mwingira, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar na Ujumbe wake kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuagana na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Efatha.Bw.Josephat Elias Mwingira, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu) 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.