Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Dkt.Mabula Aagiza Ujenzi wa Mradi Moroco Square Kikamilika Juni 30, 2022

 

Moja ya jengo katika mradi wa ujenzi wa Mji wa Kawe mkoani Dar es Salaam ambao ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani wakitoka kukagua majengo ya mradi wa Mji wa Kawe alipofanya ziara mwishoni mwa wiki.

Na Munir Shemweta, WANMM

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mkandarasi Kampuni ya Ujenzi ya Estim Construction kuhakikisha mradi wa ujenzi wa Morocco Square unakamilika kufikia Juni 30, 2022.

 

Kauli hiyo ya Dkt Mabula inafuatia serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Hassan kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukopa fedha kwa ajili ya kumaliza mradi huo uliokuwa umesimama kwa takriban miaka mitatu sasa.

 

Kwa mujibu wa Msimamizi wa mradi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Samuel Metili, mradi wa Morocco Square unaogharimu Bilioni 137.5 ulisimama tangu mwaka 2017 kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya kifedha na mabadiliko ya baadhi ya maboresho kwenye maeneo ya majengo hayo.

 

Alisema, kwa sasa ujenzi huo unaojumuisha Nyumba za Makazi kwa ajili ya kuuza na kupangisha, Maduka makubwa ya Biashara (Mall), Ofisi, Kumbi za Cinema, Mabenki pamoja na Hoteli unaendelea chini ya Kampuni ya Estim Construction na umefikia asilimia 90.

 

Naibu Waziri Dkt. Mabula alisema, haileti maana mradi huo kutokamilika mapema wakati Serikali ilishaliruhusu NHC kukopa fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo uliokwama kwa muda mrefu.

 

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa Morocco Square pamoja na ule wa Mji wa Kawe mkoani Dar es Salaam.

 

"Mradi huu wa Morocco Square umesimama kwa takriban miaka mitatu sasa, pamoja na changamoto zilizopo ninawataka mharakishe ujenzi wake na kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha 2022/ 2022 mradi huu uwe umekamilika na kuanza kutumika ili shirika liweze kupata mapato. Msimamo wa serikali ilikuwa ni kuona ile miradi iliyosimama inakamilishwa haraka na vipaumbele vilikuwa mradi wa Morocco Square na ule wa Dodoma” alisema Dkt Mabula.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Maulid Banyani alimuahidi Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa Shirika lake la NHC kwa kushirikiana na Mkandarasi watajitahidi kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika katika muda alioagiza sambamba na kuzishughulikia baadhi ya  changamoto ndani ya kipindi cha wiki moja.

 

"Mhe. Naibu Waziri naomba nikuhakikishie kuwa, tutafanya kila jitihada kwa kushirikiana na mkandarasi kukamilisha mradi huu kama ulivyoagiza na hizi baadhi ya changamoto naomba utupe wiki moja tutakuwa tumezidhughulikia" alisema Dkt Banyani.

 

Akizungumzia mradi wa Mji wa Kawe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuharakisha mazungumzo ya uwekezaji na Mwekezaji Mwenza Kampuni ya Al-Gurey-Dubai kuhusiana na mradi huo na kusisitiza kuwa, ni vizuri NHC ikawa mipango thabiti ya uendelezaji mji huo.

 

"Kuhusu mradi wa Kawe ni vizuri kujua futute plan ya eneo na ni vizuri kila eneo la Shirika la Nyumba likafanyiwa maandalizi ya kitu kinachotaka kufanyika. Yale maeneo ambayo ni 'prime' muyaainishe na kuyaendeleza maana hata NHC inaweza kunyang'anywa " alisema Dkt Mabula.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.