Habari za Punde

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ina azma ya kukiimarisha kikosi cha Zimamoto ili kukabiliana na athri kubwa zinazotokana na matukio ya moto katika Hoteli za Kitalii.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya uzinduzi mpya wa Hoteli ya Kitalii ya Tui Blue Bahari Zanzibar huko Pwanimchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya Hoteli hiyo ilioungua Jnauary 16, 2021 kufanyiwa ukarabati mkubwa na kuanza kutoa huduma.

Amesema kumekuwa na matukio mengi ya moto ya kuungua moto   hoteli za kitalii, hivyo  Serikali inajipanga kukiimarisha kikosi cha Zimamoto ili kukabiliana na hali hiyo ambayo imekuwa ikileta athari kubwa katika sekta ya Utalii.

Alisema Serikali ina kila sababu ya kuunga mkono sekta ya Utalii kwa kuzingatia kuwa hiyo ndio sekta mama ya kiuchumi.

Alieleza kuwa Uweekezaji katika sekta ya Utalii una mambo matatu yanayolinufaisha Taifa ; ikiwemo ajira, wananchi kupata soko la kuuzia bidhaa zao pamoja na Serikali kupata fedha zitokanazo na kodi, na hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali imechukua hatau mbali mbali  katika kuimarisha sekta hiyo ili kuvutia watalii, na ndio maana ikaingia mkataba na Kampuni ya ADNATA kutoka Dubai ili  kuimarisha shughuli utoaji wa huduma katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume pamoja na kuunda kikosi cha Utalii ili kuwahakikisha  watalii usalama wao wakati wanapofika nchini.

Alisema wawekezaji katika sekta ya Utalii wamekuwa wakitoa huduma mbali mbali za kijamii kwa wananchi, ikiwemo  afya, elimu na maji na hivyo akazitaka mamlaka zinazohusiana naUtalii kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha wananchi wa maenoe ya uwekezaji wananufaika ipasavyo.

Nae, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa alisema kurejea kwa huduma katika hoteli hiyo kunatokana na juhudi za mwekezaji wake kujitoa na kufanya kazi usiku na mchana na hatimae kufanikiwa kurejesha huduma hizo ndani ya kipindi kifupi na kwa kiwango bora zaidi.

Alisema kurejea kwa huduma hizo kutaimarisha sekta ya utalii kwa kutoa ajira kwa vijana, sambamba na kuchangia kikamilifu pato la Taifa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Ayoub Moahmed Mahamoud alisema miongoni mwa mafanikio ya Mkoa huo katika kukuza uwekezaji, ni pamoja na kumaliza migogoro mbali mbali, ikiwemo ule wa Hoteli ya Palolo na kubainisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Mkoa na Wawekezaji umekuwa chachu ya mafanikio hayo. 

Mapema, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali sharif alisema ufunguzi wa hoteli hiyo umekuja kutokana na Hoteli hiyo kufanyiwa matengenezo makubwa baada ya ajali ya kuungua moto  na kusababisha uharibifu mkubwa wa samani na baadhi ya majengo.

Alisema   ZIPA Inaendelea kutoa pole kwa wamiliki  wa hoteli hiyo, sambamba na kutoa pongezi kwa uongozi  kutokana na juhudi kubwa za kufanikisha  kuifanyia matengenezo Hoteli hiyo kwa zaidi ya vyumba 100.

Alisema kiasi cha Dola za Kimarekani 700,000 zimetumika kwa ajili ya uwekaji wa vifaa vya kisasa vya usalama wa hoteli ili kujikinga na majanga.

Aidha, Meneja wa Hoteli hiyo Eric Freinut aliipongeza Wizara ya Mambo ya Kale na Utalii kwa kuuunga mkono kikamilifu  juhudi za kuifanyia matengenzo makubwa hoteli hiyo hadi kurejea katika hali yake ya kawaida.

Hoteli ya Tui Blue Bahari Zanzibar, ni hoteli ya kitalii ya nyota  tano inayomilikiwa na Kampuni ya Zanzibar Beach Village ilioanza na uwekezaji mwaka 2007 , ambapo uwekezaji huo ulianza na mtaji na Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 17 na kuongezeka hadi kufikia Dola Milioni 47 kabla ya ajali ya kuunga moto.Hoteli hiyo imeajiri wafanyakazi 258 kati ya hao ni 17 pekee ndio wageni.

                                                                              

Imetayarishwa na

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.