Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa Aipomgeza UVCCM *Asema michuano ya UVCCM GREEN CUP imewaunganisha vijana na kuibua vipaji

Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa Akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kenani Kihongosi alipokuwa mgeni rasmi katika mchezo wa fainali wa UVCCM GREEN CUP uliozikutanisha Timu ya mpira wa miguu ya Mkoa wa  Magharibi (Zanzibar) na Timu ya mpira wa miguu ya mkoa wa Pwani (Tanzania Bara)  kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam, Desemba 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Kassim Majaliwa ameupongeza Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kwa ubunifu wa kuanzisha michuano ya UVCCM GREEN CUP ambayo imeleta vijana wa Tanzania nzima sehemu moja.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa michezo hiyo ambayo ilishirikisha timu 32 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa mpira wa miguu na pete itasaidia kuibua vipaji ambavyo vitakuja kuzitumikia timu zetu za Taifa.

 

Amesema hayo leo Jumapili (Desemba 12, 2021) aliposhuhudia mchezo wa fainali ya mpira wa miguu kati ya Mkoa wa Magharibi (Zanzibar) na Mkoa Pwani (Tanzania Bara) jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo timu ya Mkoa wa Magharibi iliifunga timu ya Mkoa wa Pwani kwa magoli 3-1

 

Waziri Mkuu ameushauri Umoja Vijana kuiingiza  michezo hiyo kwenye ratiba ya UVCCM taifa ili kila tarehe 9 Desemba ya kila mwaka iwe ni michezo kwa vijana nchi nzima kaunzia ngazi ya wilaya hadi Taifa “lengo ni kuibua vipaji vya vijana wetu na kuwaunganisha”

 

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kenani Kihongosi amesema kuwa Umoja  wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi uliona ni muhimu kuanzisha michuano ya UVCCM GREEN CUP kwa ajili ya kuanda na kukuza vipaji vya mpira wa miguu na pete “Lengo lingine la michuano hii ilikuwa pia ni kutunza mazingira na kuimarisha afya”

 

Kihongosi aliongeza kuwa kupitia michuano hiyo wameweza kukuza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa vijana walioshiriki michuano hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini

 

Mshindi wa kwanza wa michuano hiyo kwa upande wa mpira wa pete ni mkoa wa Dar es Salaam na nafasi ya pili ilishikwa na Mkoa wa Mjini Magharibi.

 

Kadhalika, Umoja wa Vijana umekabidhi tuzo Maalumu kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kitambua mchango wake na malezi bora kwa Jumuiya na Chama.

 

(Mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, DESEMBA 12, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.