Habari za Punde

Kampuni ya IHC ya Abu Dhabi yaahidi kuwekeza Zanzibar

 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE                  


Abudhabi                                                                                                                                                                                                      19.01.2022

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na uongozi wa Kampuni ya ‘International Holding Company (IHC) yenye makao yake Abudhabi.

Kampuni hiyo ni kubwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na ya pili kwa nchi za Magharibi ambapo katika mkutano huo Abudhabi imeahidi kuleta wawekezaji wa kigeni hapa Zanzibar.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Kampuni ya ‘International Holding Company (IHC) uliopo Mjini Abudhabi.

Rais Dk. Mwinyi katika mazungumzo hayo aliwaeleza kwa undani wawekezaji hao wa Kampuni ya (IHC) fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu na kuwaalika kuja Zanzibar.

Alisema kuwa Zanzibar kwa sasa inahitaji wawekezaji makini huku akieleza kwamba moja ya fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu ni uwekezaji katika visiwa vidogo vidogo vinavyofikia 53 katika bahari ya Zanzibar

Fursa nyingine zinazoambatana na uwekezaji wa Uchumi wa Buluu alizozieleza Rais Dk. Mwinyi ni pamoja na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, uvuvi mkubwa katika bahari kuu, ujenzi na kuzifanyia matengenezo meli za uvuvi, ujenzi wa bandari kubwa zitazoweza kuhimili meli kubwa za mizigo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kwamba yote hayo yatafanikiwa iwapo kutakuwa na miundo mbinu mizuri katika huduma za kijamii na kuwaeleza wawekezaji hao umuhimu wa kusaidia huduma za kijamii za elimu na afya na kuanzisha mikakati maalum ya kiuchumi

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Shariff Ali Shariff akitoa muelekeo wa fursa za uwekezaji kwa waekezaji hao aligusia hali ya watalii  ilivyo Zanzibar ambapo licha ya ugonjwa wa UVIKO- 19, Zanzibar iliendelea kupokea watalii 39,512 kati ya mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana.

Alieleza kuwepo kwa fursa za kuwekeza katika kuchakata bidhaa za baharini, ujenzi wa boti za uvuvi pamoja na kuzifanyia matengenezo, ujenzi wa mji mwengine utakaoitwa Zanzibar Marina City na kusaidia kilimo cha mwani.

Pia, alieleza haja kwa wawekezaji hao kuisaidia Zanzibar kuwa na kituo cha kukuza vipaji kwa michezo mbalimbali hali itakayoipaisha Zanzibar katika sekta ya michezo.

Mkurugenzi huyo wa (ZIPA), alibainisha kuwepo kwa hekta 6000 za ardhi inayohitaji kuendelezwa katika eneo la Makurunge, ardhi ambayo ni mali ya Zanzibar na inafaa kwa ajili ya kilimo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje Sheikh Shajkboot Nahyan Al Nahyan ambapo walizungumza mahusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia ufunguzi wa Ubalozi Mdogo wa (UAE) Zanzibar pamoja na kurejesha huduma za ndege za (UAE) na kufanya safari zake Zanzibar.

Ziara ya Rais Dk. Mwinyi inamalizika leo Jumatano Januari, 19, 2022 na anatazamiwa kuondoka Abudhabi jioni na kurejea Zanzibar.

 

Imetayarishwa na kitengo cha habari

Ikulu zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.