Habari za Punde

Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi Ametoa Msamaha kwa Wanafunzi 29 Waliokuwa Wakiendelea na Vyuo Vya Mafunzo Unguja na Pemba.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa msamaha kwa wanafunzi ishirini na tisa (29) ambao walikuwa wakiendelea kutumikia Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa Sherehe za miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said ilieleza kwamba msamaha huo unatokana na uwezo aliopewa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba wanafunzi hao waachiwe huru kuanzia tarehe 11 Januari 2022, ambapo tayari wanafunzi hao wameshaachiwa huru tokea tarehe hiyo.

Taarifa hiyo, imeeleza kuwa, kwa kuwa Zanzibar ilisherehekea miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo tarehe 12 Januari 2022, na kwa kuwa Rais aliridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hiyo, basi wanafunzi hao waachiwe huru.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni  Vuai Juma Makame, Abdalla Juma Abdalla, Mrisho Moh’d Mrisho, Vuai Matogo Vuai, Said Rashid Khamis, Foti Joseph Magingi, Vuai Hassan Moh’d, Juma Omar Risasi, Omar Ali Omar, Abdalla Malik Moh’d, Mohamed Khamis Mohamed, Makame Mdungi Makame, Amar Shukuru Hamad, Sadam Hussein Tajo, Khalfan Mzaka Khalfan na Abdalla Moh’d Marijani.

Aidha, wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni  Suleiman Khamis Suleiman, Moh’d Rajab Hamad, Hafidh Ali Abdalla, Yussuf Shaib Juma, Ali Bakari Suleiman, Omar Juma Ali, Abdalla Omar Suleiman, Twahiru Muhsin Salim, Sultan Hassan Khatib, Ramadhan Hassan Soud, Haji Omar Haji, Hashim Moh’d Khamis na Khamis Sheha Idd.

Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi matukufu, huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakisha muda mfupi wa kutumikia chuoni sambamba na  kuonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.

Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya Umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.