Habari za Punde

Dkt. Gwajima Awapongeza Ngariba Walioacha Kukeketa Awaahidi Ushirikiano na Serikali.

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum.Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima, amewapongeza Ngariba waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ukeketaji baada ya kuacha kufanya vitendo hivyo na kisha kugeuka kuwa wanaharakati wa kukemea vitendo vinavyo dhalilisha utu wa mtoto wa kike na kumuachia maumivu makali.


Na WMJJWM- Tarime Mara

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewapongeza Ngariba waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ukeketaji baada ya kuacha kufanya vitendo hivyo na kisha kugeuka kuwa wanaharakati wa kukemea vitendo vinavyo dhalilisha utu wa mtoto wa kike na kumuachia maumivu makali.

Akifunga Kongamano Maalum kwajili ya mapambano ya kutokomeza Ukeketaji lilichofanyika mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, Dkt. Gwajima alisema, kitendo cha Ngariba hao kuacha suala la Ukeketaji na kujiunga na Serikali katika mapambano hayo ni ujasiri wa hali ya juu na nicha kupongezwa.

“Mmewasikia wenyewe wakijieleza hapa, kwamba wapo baadhi yao walikata shauri na kuacha kuendelea kukeketa, lazima tuwapongeze sana kwa hatua hii. Lakini baadhi yao wanatishiwa hata kutengwa na jamii zao baada ya kuacha vitendo hivyo vya kikatili, tuseme kama Serikali na wadau tutakuwa nao bega kwa bega kuwatetea kwa nguvu zote bila kuchoka” alisema Waziri Dkt. Gwajima.  

Dkt. Gwajima alisema dhana ya kwamba, mtoto kumvusha rika kutoka usichana kwenda kuwa mama au mtu mzima sio lazima akeketwe zipo njia mbadala za kumvusha binti rika ikiwepo kuwapatia mafunzo yakujitambua bila kumuathiri mwili wake.

Ameongeza kuwa, zipo athari wanazo kumbana nazo Mabinti wanaokeketwa ikiwepo athari za kisaikolojia na msongo wa mawazo, kwani, vitendo hivyo hufanywa bila ridhaa ya wahusika, kupata maumivu makali, kutokwa damu nyingi, kuuguza kidonda, changamoto za kujifungua na uwezekano wa kupoteza maisha. 

“Madhila mengine kusababisha maambukizi ya magonjwa ya ngono, Virusi vya UKIMWI pamoja na magonjwa ya njia ya mkojo (UTI), lakini pia uwepo wa kovu la ukeketaji linalo kusababisha mimba kinzani na unaweza kusababisha fistula”. alisisitiza Dkt. Gwajima, na kuongeza kuwa, 

“Mtoto anaweza kupata changamoto wakati wa kujifungua ambapo zinaweza kumsababishia mtindio wa ubongo, na kupata mateso katika maisha yake yote. aliongeza Waziri Dkt. Gwajima.

Awali kabla ya kufunga mafunzo hayo, wakichangia mada zilizowasilishwa katika Kongamano husika, Mangariba hao waliiomba Serikali iwalinde, ili wasikutwe na madhila kutoka ndani ya Jamii zao.

“Tunapo acha shughuli za Ukeketaji ni kama tumetangaza vita na wazee wa Mila, lakini pia Jamii zetu, hivyo Mhe. Waziri, tunaomba sana, tunapo salimisha zana za Ukeketaji, basi Serikali itungalie namna inavyoweza kutuwezesha ili tuwe na mitaji na kufanya shughuli mbadala, lakini zaidi sana, tunaomba tulindwe dhidi ya wanaotutishia, alisisitiza mmoja ya Ngariiba.

Nao viongozi wa Dini ambao walikuwa Sehemu ya Kongamano hilo, wameitaka Serikali kubadili mtazamo wa elimu na kutaka elimu husika izidishwe kwa watoto wa kiume kwani pamoja na kuwachukuwa Wasichana na kuwapeleka katika makaazi salama kwa wale wanaokimbia vitendo hivyo, kazi bado ipo kwa wavulana ambao hawana Elimu ya madhila ya ukeketaji kwa mwanamke

“Ndugu Viongozi na Washiriki wa Kongamano hili, kwa sasa tumewekeza angalau kwa watoto wa kike, lakini kuna kundi kubwa la wavulana, hawa tumewaweka nyuma, niiombe Serikali na Wadau, tulitazame kundi hili, alisema” Sheikh Khalfan Shaban Mtongori.

Kila mwaka, mwezi Februari, Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa Wanawake na Watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.