Habari za Punde

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa EAC Wasisitiza Umuhimu wa Upatikanaji wa Nishati ya Uhakika.

 

Waziri wa Nishati Mhe.Januari Makamba akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mkutano uliofanyika Jijini Arusha leo 11 Febuari 2022.

Waziri wa Nishati Tanzania Mhe. Januari Makamba (wa kwanza kulia) pembenbi yake ni Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Peter Mathuki, Mawaziri wa Nishati wa Uganda na Kenya pamoja na Viongozi wengine Waandamamizi wa Nishati walioshiriki mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta ya Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mkutano uliofanyika leo 11 Febuari 2022 Jijini Arusha Tanzania.

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 11 February 2022 jijini Arusha, Tanzania kwaajili ya kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo.

Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ya awali ngazi ya Wataalamu/Maafisa waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari 2022 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 10 Februari 2022.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye ameambatana na; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati - Tanzania Bara, Mhandisi Felschesmi Mramba; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar; Dkt. Mgereza Miraji; Dkt. Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati; na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa ujumla.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Makamba aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo nchini na kuwahakikishia kuwa mkutano utafanikiwa kuyafikia malengo yake kufuatia uongozi imara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.

Vilevile akaeleza ukanda wa Afrika Mashariki umejaaliwa rasilimali nishati za kutoka hivyo, ni wakati sasa kwa kila nchi kuwa na mikakati imara ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kuihakikishia jamii upatikanaji wa huduma zote zinazohitaji nishati.

“Tukiwa tunapitia changamoto za ugonjwa wa COVID-19 tumeshuhudia namna gani nishati ya umeme na gas zilihitajika katika kusaidia kuleta nafuu na kuokoa maisha ya wananchi wetu” alisema Mhe. Makamba.

Naye mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Monica Juma alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watalamu na Mkatibu Wakuu kwa kufanya maandalizi mazuri ya Mkutano huo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni moja ya viashiria vya kukua kwa uchumi wa nchi yeyeote.

Pia akaeleza kukua kwa uchumi husaidia kupunguza utegemeze na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuziwesha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uzalishaji wa kutosha viwandani na katika sekta ya kilimo.

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Nishati pamoja na mambo mengine utapitia na kutoa maamuzi juu ya; Tarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Jadidifu, Nishati ya Umeme na Nishati ya Mafuta; pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika mkutano huu utajadili kwa kina utekelezaji wa mradi wa kituo cha Nishati Jadidifu cha Afrika Mashariki; Mradi wa Kufua Umeme wa Nsongezi; Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kigagati (14MW) na Taasisi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati katika Nchi za Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.