Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi ahimiza kuzingatia haki na uadilifu kwa watumishi wa umma

 


                               STATE HOUSE ZANZIBAR

                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                          PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                        Februari 18, 2022

 

Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia haki na uadilifu kwa kutambua dhima kubwa waliyonayo kwa Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dk Mwinyi amesema hayo kwa waumini wa Dini ya kiislamu baada ya kukamilika kwa sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Al - Qudus uliopo Kijitoupele Jijini Zanzibar.

Alisema watumishi wa  umma wana wajibu wa kufanya kazi  kwa kuzingatia uadilifu na kutambua nafasi walizokabidhiwa ni dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hivyo wanapaswa kufanya haki na kuondokana na dhulma.

Aliwataka watumishi hao kuondokana na dhana iliojengeka miongoni mwao kuwa mali ya Serikali haina mwenyewe.

Alisema Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi za maendeleo, hivyo akatowa wito kwa wafanyakazi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara kuwa waadilifu, hususan katika suala la ulipaji wa kodi.

“Wafanyakazi wa Serikali na wafanyabiashara  sote tufanye kazi ya kuisaidia Serikali “, alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kufahamu kuwa shughuli mbali mbali za maendeleo zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbali mbali ya nchi pamoja na hatua za kuwajibisha  Watendaji wa Serikali, zinafanyika kwa nia njema ili kuleta ustawi  mwema wa taifa.

Alhaj Rais Dk. Mwinyi alishangazwa na mitazamo ya baadhi ya wananchi kuhusiana na uzungushwaji wa mabati katika maeneo ya miradi mbali mbali inayoendelezwa na kusema hayo yanafanyika kwa nia njema kwa lengo la kuliletea Taifa maendeleo, kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo elimu na afya.

“Nia na dhamira ya Serikali ni njema,……. ni kujenga nchi”, alisema.

Alhaj Dk. Mwinyi alirejea kauli yake ya kuwaomba Wazanzibari kuendelea kumuombea dua ili aweze kutekeleza yale yote aliyoyaahidi pamoja na kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yake.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewataka  wananachi kwa ujumla kuwa na imani na Viongozi wao wakati huu wakitekeleza ahadi, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi..

Mapema Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumma, Sheikh Idd Hussein  aliwataka waislamu kujikita katika kutafuta uchamungu kwa kufanya mambo mema na kubainisha mambo manane muhimu, ikiwemo la  suala la uadilifu katika dhamana wanazokabidhiwa.  

Katika hatua nyengine, Rais Alhaj Dk.Mwinyi alifika nyumbani kwa Mzee Bwanakheir Omar kwa ajili ya kumjuilia hali huko Kiembesamaki Jijini Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.