Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amewata WanaCCM Kujibu Hoja kwa Vitendo Badala ya Maneno.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wanaCCM kujibu hoja kwa vitendo badala ya maneno kwani wanadhima kubwa ya kuendeleza amani iliyopo nchini.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa CCM Amani Mkoa, katika uzinduzi wa Kongamano la Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wazazi Tanzania, ambalo kitaifa mwaka huu linafanyika hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba hivi karibuni wametoa baadhi ya watu kuanza maneno maneno juu yake na Serikali anayoiongoza na kusema kwamba ni vyema watu hao wakajibiwa kwa vitendo badala ya maneno.

Rais Dk. Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliwataka wanaCCM kuwa na subira huku Serikali anayoiongoza ikitekeleza majukumu yake ipasavyo sambamba na chama chao kikiendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa vitendo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali zote mbili ziznathamini kazi nzuri inayofanywa na Umoja wa Wazazi Tanzania kwnai wakati wote wameonesha kuguswa na hatua za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuifuatilia na kutoa ushauri kila unapohitajika.

Kadhalika Jumuiya hiyo imekuwa ikiendeleza jukumu la kusimamia elimu na maadili kwa watoto, malezi na utamaduni wa Taifa kwa mujibu wa Sera na Ilani ya CCM kote Tanzania Bara na Zanzibar.

Aliupongeza Umoja wa Wazazi Tanzania kwa kusimama kidete katika kuitafsiri kwa vitendo kaulimbiu yake ya “Uchungu wa Mwana Aujuae Mzazi”, kwa kuwa mstari wa mbele  katika kushirikiana na Serikali zote mbili katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na wanawake pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

“Kwa namna mbali mbali mmeendelea kutukumbusha wazazi wajibu wetu wa kuwapa watoto wetu malezi bora yanayoendana na maadili yetu, silka na utamaduni wetu ili kukipa kizazi chetu urithi sahihi utaowajenga kuwa wazalendo na raia wema wa nchi hii”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipongeza kwa kuwepo mada inayohusiana na Uchumi wa Buluu na kutoa wito kwa washiriki wa Kongamano hilo  kufuatilia kwa umakini taaluma itakayotolewa na wataalamu kuhusu Uchumi wa Buluu ili wakitoka hapo wakawe walimu wa wananchi wengine waliokosa fursa ya kuwepo katika Kongamano hilo.

Pia, alisisitiza katika kufanikisha malengo ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM),  ni lazima kuendeleza utaratibu wa kufanya ziara katika ngazi za chini walioko wanachama wao ili kuweza kuzifahamu changamoto zao na hatimae kuzipatia ufumbuzi.

Alitoa wito kwa wananchi kushiriki katika zoezi la sensa  wakati utakapofika kwa kutoa ushirikiano na kuwapa taarifa sahihi maofisa watakaohusika na zoezi hilo.

Nae Mwenyekiti wa Wazazi Taifa Edurmund Mndolwa alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuiletea maendeleo Zanzibar na kuahidi kwamba Umoja wa Wazazi utaendelea kumuunga mkono.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alitoa pongezia kwa Jumuiya hiyo kwa kufanya Kongamano hilo ambalo lina umuhimu mkubwa katika kukiendeleza chama hicho huku akisisitiza suala zima la kuendeleza amani nchini.

Katika kongamano hilo mada mbali mbali zimetolewa ikiwemo Uchumi wa Buluu, historia ya Umoja wa Wazazi pamoja na udhalilishaji wa kijinsia.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alikabidhiwa zawadi yake na Jumuiya hiyo pamoja na kukabidhiwa zawadi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzabnia Samia Suluhu Hassan ambayo alipokea kwa niaba yake.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.