Habari za Punde

Makarani , Wasimamizi wa Sensa Kupatikana Ndani ya Mikoa Husika

Na. Lilian Lundo - MAELEZO

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kwamba, utaratibu wa kuwapata makarani na wasimamizi wa sensa utasimamiwa na kamati za sensa za mikoa.

Dkt. Chuwa amesema hayo leo, Machi 28, 2022, Jijini Dodoma, alipokuwa akitolea ufafanuzi wa uvumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) zimetangaza nafasi za kazi za makarani na wasimamizi wa sensa.

“Kazi ya kuwapata makarani na wasimamizi wa Sensa itasimamiwa na kamati za sensa za mkoa ambazo wenyeviti wake ni wakuu wa mikoa husika. Nia ya serikali kufanya hivyo ni kuhakikisha watu wote wanaotaka kufanya kazi za ukarani na usimamizi wa sensa watoke katika maeneo yao wanayoishi,” alifafanua Dkt. Chuwa.

Aliendelea kusema kuwa, hadi sasa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) hazijatangaza nafasi za kazi za wasimamizi na makarani wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022.

Dkt. Chuwa ametoa tahadharia kwa wananchi kuwa, kuna tovuti inatangaza kuwepo kwa nafasi za kazi za makarani wa sensa na tayari baadhi ya watu wameshasajiliwa kwenye mfumo wa malipo. Aidha amesema kuwa, NBS na OCGS haijaanzisha tovuti ya https://www.sensatanzania.com, hivyo tovuti hiyo si rasmi na haitambuliki na serikali.

Ameendelea kusema kuwa, nafasi za ukarani na usimamizi wa Sensa zitatangazwa rasmi kupitia tovuti na mitandao ya kijamii ya NBS na OCGS, redio, runinga na magazeti mara baada ya taratibu zote za serikali zitakapokamilika.

“Watanzania wote wenye nia ya kuomba nafasi hizo wafuatilie mawasiliano rasmi ya serikali ikiwemo tovuti za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) www.nbs.go.tz na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) www.ocgs.go.tz, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Kata na Tarafa,” alifafanua Dkt. Chuwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.