Na Raya Hamad OMKR
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak amesema
lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kutoa fursa na haki kwa Watu wenye
Ulemavu na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo jumuishi yanayozingatia mahitaji
ya watu wote na kuzingatia mahitaji Watu wenye Ulemavu
Ameyasema hayo kwenye mafunzo ya maendeleo jumuishi kwa Wakurugenzi
mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwemo wakurugenzi Uendeshaji
na Utumishi pamoja na Wakurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara na taasisi
za Serikali kwenye ukumbi wa mkutano wa Hoteli ya Madinatul Bahri
Dkt Shajak ameeleza kuwa umuhimu wa mafunzo hayo kupewa wakurugenzi kwa
vile wao ndio moja kati ya kiini katika kila wizara kwa vile wao ndio waratibu
watengeza sera, waendeshaji na ndio wanaozalisha mipango ya serikali,
wanaotengeneza sera na kusimamia tafiti mbalimbali pamoja na ajira
Aidha Dkt Shajak amewasihi wakurugenzi hao kuhakikisha wanazingatia
huduma stahiki na nzuri wanazotakiwa kupatiwana Watu wenye Ulemavu na kuona
kila penye fursa kunakuwa na mazingatio kwa Watu wenye Ulemavu ili lengo la
serikali la kutoa haki na fursa liwe linatekelezwa kwa mujibu wa taratibu
“Nitowe mfano kwa baadhi ya
taasisi ambazo zinaajiri mfanyakazi akiwa hana ulemavu na anapopata ulemavu
akiwa kazini si busara kumhamishia kwenye taasisi inayosimamia masuala ya Watu
wenye Ulemavu bali unachotakiwa kusimamia na kuhakikisha anapata huduma, haki
na fursa kulingana na ulemavu wake” alisisitiza Dkt Shajak
Nae Mkurugenzi wa Bi Salma Majid ameishukuru Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kwa mashirikiano makubwa wanayoyapata ikiwemo Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais jambo ambalo limewarahisishia kufikia malengo ya mradi yenye
tija na kuelekea Sera ya Serikali ya uchumi wa buluu na kuona Watu wenye
Ulemavu wanashirikishwa kwenye masuala ya maendeleo ya kiuchumi katika nchi yao
Mradi wa Mafunzo ya Maendeleo Jumuishi katika Jamii unatekelezwa na
zaidi ya nchi 100 duniani ikiwemo
Zanzibar na kuendeshwa kwa ushirikiano wa watu wenye ulemavu, familia zao, na
jamii taasisi za serikali na zisizo za kiserikali zinazohusiana na utoaji wa
huduma za afya, elimu, mafunzo ya amali, huduma za jamii na nyenginezo
Wakitoa ushuhuda kwenye mafunzo hayo juu ya mtazamo wa wanajamii mwalimu
wa skuli ya sekondari Mpendae Bi Yumna Mmanga amesema yeye ni mwalimu anaefurahiya
kazi yake kwa sababu wanafunzi wake wanajifunza namna nzuri ya kuishi na Watu
wenye Ulemavu na kufahamu mahitaji yao, matumizi sahihi ya majina ya Watu wenye
Ulemavu na namna ya kuwaita
“naishi nao kirafiki zaidi, napenda wamekuwa wadadisi, na waelewa jambo
ambalo linanipa faraja katika kutekeleza majukumu yangu hawanitengi ingawa
ninapotembea wakati mwengine wengine hutaka kupiga picha nami wakijua ni mzungu
kumbe ni mwanamke mrembo kama wanafunzi wangu wanavyoniita mwalimu mrembo”
alisema Yumna
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo Mkurugenzi uendeshaji na Utumishi
Bakari Khamis kutoka Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora kwa
niaba ya Wakurugenzi wameishukuru Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais kupitia
Baraza laTaifa la Watu wenye Ulemavu kwa kuandaa mafunzo hayo jambo ambalo
linatoa fursa kwa wakurugenzi kufahamu na kuelewa vyema masuala ya Watu wenye
Ulemavu na namna ya ushirikishwaji wao
Nae Mkurugenzi Mipango, sera na utafiti kutoka Wizara ya uchumi wa buluu
na uvuvi Bw Sheha I. Hamdan amesema mafunzo yamekuja kipindi muwafaka cha
bajeti ya Serikali kinachopanga mipango ya maendeleo hivyo wanawajibu wa
kuhakikisha wanazingatia masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa kuweka mazingira
wezeshi ili dhana nzima ya uchumi wa buluu kwa wote iweze kufikiwa
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia
Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana Mradi wa Mafunzo ya
Maendeleo Jumuishi katika Jamii, yalitanguliwa na Makatibu wakuu wa Wizara na
Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo yaliendeshwa na Mwenyekiti
wake Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena A. Said yakifuatiwa na Wakurugenzi
ambayo yaliongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D.
Shajak
Mada zilizowasilisha ni pamoja na kufahamu dhana ya ulemavu na
uzingatiaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa
Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na Dkt Said Khamis kutoka Chuo cha Taifa
SUZA ambapo pia washiriki walifahamu aina za ulemavu na sababu zinazopelekea
kupata ulemavu
No comments:
Post a Comment