Habari za Punde

Waziri Mhe.Balozi Dkt.Chana Azindua Ujenzi wa Majengo ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana (wa tatu kulia) akimkabidhi mkataba wa ujenzi wa majengo hayo mkandarasi Bwa. Ding Wu Machi 25, 2022 Kisasa Jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu-Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi. Dkt.  Pindi Chana amezindua ujenzi wa mradi wa majengo ya Idara ya MpigaChapa Mkuu wa Serikali utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 hadi kukamilika  kwake majengo yatakayotumika kuzalisha nyaraka za Serikali.

Mhe. Waziri Pindi aliyasema hayo Machi 25, 2022 wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la ujezi huo lenye ukubwa wa mita za mraba 47,214 kwa mkandarasi wa ujenzi huo Hainan International Limited yatakayojengwa Kisasa Jijini Dodoma ambapo alisema kulingana na mkataba wa ujenzi mradi huo unatakiwa kukamilika  kwa kipindi cha miezi 12.

 Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Ofisi ya Waziri Mkuu ilidhinishiwa fedha za maendeleo ya ndani shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya MpigaChapa mkuu wa serikali.  

“Ujenzi wa majengo haya utahusisha ujenzi wa jengo la kiwanda, jengo la Ofisi, jengo la Canteen, ujenzi wa duka la vitabu la serikali na ujenzi wa uzio hivyo mradi unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha ambapo mwaka wa fedha 2021/2022 ujenzi utakaofanyika ni wa jengo la kiwanda  kwa gharama za shilingi bilioni 2.29,”alisema Mhe. Pindi.

Akizungumzia kuhusu Mshauri Elekezi alifafanua kuwa ni kampuni  ya Aru Built Environment Company Limited kwa gharama za shilingi milioni 389.5 zikijumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Aidha alimtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa mkataba unavyoelekeza hatua ambayo  itasaidia kufanyika kwa shughuli za uzalishaji wa nyaraka muhimu za Serikali kama ilivyokusudiwa huku akisisitiza Mshauri Elekezi kuhakikisha anasimamia mradi kwa ubora na viwango kwa mujibu wa mkataba.

“Utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati wa malengo haya ya maendeleo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu utafanyika chini ya mkataba yaani miezi 12 na mkandarasi ndiye mtekelezaji wa mradi huu azingatie  maelekezo na miongozo  ya ujenzi wa mradi kwa ukamilifu,”Alifafanua Mhe. Waziri Pindi.

 “Muda wa maandalizi ya kuanza kazi ni wiki mbili kuanzia tarehe Machi 25,2022 kuanza rasmi ni April 08,2022 na kukabidhiwa mradi ni  ifikapo Machi 07,2023,”alihimiza.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Hainan International Limited kutoka Nchi ya China, Mhandisi Ding Wu aliahidi atahakikisha watanzania wanapewa kipaumbele cha ajira katika mradi huo ili kukuza uchumi wao na kuchangia pato la Taifa.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini na kutupa kazi hii kama Waziri alivyotuelekeza sisi tuna uhakika hii kazi tutamaliza ndani ya muda  ikiwa na ubora ambao Serikali inataka kulingana na fedha iliyotolewa na kwa sisi mipango yetu hatutaki kazi ifike miezi 12 ndani ya miezi 10 tutakuwa tumemaliza na kukabidhi,”alishukuru Mhandisi Wu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la Ujenzi wa Majengo ya MpigaChapa Mkuu wa Serikali kwa Mkandarasi Hainan International Limited
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu) Bwa. Kaspar Mmuya akifafanua jambo katika  hafla ya kukabidhi eneo la Ujenzi wa Majengo ya MpigaChapa Mkuu wa Serikali kwa Mkandarasi Hainan International Limited
Mwakilishi wa Kampuni ya ABCC ambaye pia ni Meneja wa Mradi Oliver Gonda (wa kwanza kushoto) akitoa maelekezo ya ramani ya majengo hayo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi. Dkt. Pindi  Chana (aliyekaa wa pili kulia) na Mratibu Mkuu wa Ufundi Bwa. Saudeni Anania (aliyesimama).





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.