Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ametuma Salamu za Rambirambi kwa Rais wa Kenya Mhe Uhuru Kenyata.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya  Kenya Uhuru Kenyata kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Taifa hilo Mwai Kibaki.

Katika salamu hizo Rais Dk. Mwinyi alieleza jinsi alivyopokea kwa mshituko na huzuni kubwa kifo cha Rais Mwai Kibaki ambaye alikuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya tangu mwaka 2002 hadi 2013.

Salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wote wanaungana na ndugu zao wa Kenya katika kipindi hichi cha msiba na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze Marehemu Kibaki mahala pema peponi. Amin.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimnasihi Rais Uhuru Kenyata pamoja na wananchi wote wa Kenya kuendelea kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Rais Mwai Kibaki atakumbukwa kwa juhudi zake kubwa alizozichukua katika kuuimarisha uchumi pamoja na demokrasia ya  Kenya.

Rais Uhuru Kenyata alitangaza kwamba, Rais Kibaki (90) amefariki dunia usiku wa siku ya Alhamis ya tarehe 21.04.2022.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.