Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amelipongeza Shirika la Fedha Duniani IMF Kwa Kuimarisha Uchumi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mshauri wa Shirika la Fedha Duniani ( IMF) Masuala ya Maendeleo Barani Afrika.Mr.Charalambos G.Tsangarides (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo akiongozana na Ujumbe wake,mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 6-5-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Mshauri wa Shirika la Fedha Duniani ( IMF) Masuala ya Maendeleo Barani Afrika Mr.Charalambos G.Tsangarides.(kulia kwa Rais) wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 6-5-2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa kuendelea kuinga mkono Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ukiongozwa na Mshauri wa Shirika hilo wa masuala ya maendeleo Barani Afrika Charalambos Tsangarides.

Katika maelezo hayo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Shirika la (IMF) limekuwa ni msaada mkubwa kwa Zanzibar kutokana na juhudi zake inazoendelea kuzichukua katika kuiunga mkono Zanzibar hasa katika kipindi hichi ambacho uchumi wa dunia umedorora.

Alieleza kuwa mkopo fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Shirika hilo kwa Zanzibar  ulikuwa na umuhimu mkubwa na kuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Zanzibar katika kipindi ambacho uchumi wake ulitetereka kutokana na janga la maradhi hayo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inafaa kupongezwa kwani ilisaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na wakati ambapo sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar iliathirika kutokana na janga la Uviko- 19.

Alifahamisha kwamba kuathirika kwa sekta ya utalii ilipelekea kuiathiri sana bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na sekta hiyo kuwa ndiyo muhimili mkuu wa uchumi ambayo ina mchango mkubwa katika bajeti pamoja na pato la Taifa.

Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe huo kwamba mkopo huo wa Uviko-19 uliotolewa na (IMF) uliweza kuchangamsha uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alitumia fursa hiyo kulishukuru Shirika hilo la Fedha Duniani (IMF), pamoja na timu hiyo iliyofika Zanzibar kwa azma yake ya kuendelea kuisaidia Zanzibar katika awamu ya pili ambapo fedha zitakazopatikana katika mkopo huo zitalenga kuendeleza yale yote yaliyoanzwa katika mkopo wa awali ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa fedha hizo pia, zitasaidia katika kufufua uchumi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele vya Serikali pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi hasa katika maeneo ya masuala ya bajeti pamoja na takwimu.

Nae Mshauri wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), katika masuala ya maendeleo Barani Afrika Charalambos Tsangarides alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi pamoja na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuutumia vyema mkopo huo.

Katika mazungumzo hayo, Mshauri huyo wa Shirika la (IMF), wa masuala ya maendeleo Barani Afrika alieleza kuridhika kwake na juhudi zilizochukuliwa na Zanzibar katika kuhakikisha mkopo uliotolewa na Shirika hilo unatekeleza vyema shughuli zilizokusudiwa.

Bwana Tsangarides alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi Shirika hilo lilivyopata hamu ya kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuongeza awamu ya pili ya fedha za mkopo ambazo zitasaidia kuendeleza miradi ya maendeleo sambamba na kukuza uchumi wa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Mshauri huyo alieleza hatua mbali mbali zitakazochukuliwa na (IMF) katika kuhakikisha Zanzibar inafaidika moja kwa moja na fedha hizo ili kuweza kurahisisha shughuli zake za kiuchumi na kimaendeleo.

Imetayarishwa na Idara Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.