Habari za Punde

Dkt.Nchemba Azungumza na Wadau wa Mpira wa Miguu na Kujadili Maendeleo ya Soka Nchini.Na Scola malinga, WFM, dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Yanga Bw. Senzo Mbatha, baada ya kumalizika kwa mkutano wake na viongozi wa vilabu vya mchezo wa mpira wa miguu nchini, kupitia Bodi ya Ligi, mkutano huo ulifanyika katika Ofisi  Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Na Scola Malinga, WFM, dar es Salaam                                                                                               

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na vilabu vya michezo pamoja na taasisi za Serikali zinazosimamia sekta hiyo ili kujadili mipango na mikakati ya kuendeleza sekta ya michezo nchini. 

Wadau hao walimweleza Dkt. Nchemba kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika kuendeleza soka ikiwemo ufinyu wa bajeti katika Vilabu vyao pamoja na kuiomba Serikali iendelee kutoa nafuu zaidi ya kodi kwenye nyasi bandia pamoja na viunganishi vyake.

Dkt. Nchemba amewahakikishia wadau hao kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Rais samia Suluhu Hassan aliyowapa ni kuhakikisha kuwa Sekta ya michezo inakuzwa kwa kuwa ni muhimu na vijana wengi wamejiajiri kupitia sekta hiyo.

Alitoa wito kwa vyama vinavyosimamia michezo nchini kuhakikisha kuwa sekta hiyo inafanya vizuri ili kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi pamoja na kuhakikisha kuwa miundombinu ya viwanja inajengwa kwenye maeneo ya kimkakati ili kukuza michezo nchini.

Aidha, Dkt. Nchemba amewaangiza wataalum wa Wizara ya Fedha na Mipango wapitie changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wadau pamoja na kuzipitia sharia za kodi ili kuendeleza sekta hiyo wakati huu ambapo bajeti ya Serikali inajadiliwa bungeni.

Akizungumza kwa niaba ya vilabu hivyo vya mpira wa miguu nchini, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi na Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Steven Mnguto,  aliishukuru Serikali kwa kuthamini michezo na kuomba changamoto walizoziwasilisha kwake zifanyiwe kazi ili soka la Tanzania liweze kupiga hatua zaidi na kuzipa nafuu klabu ili ziweze kujiendesha.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba Bi. Barbara Gonzalez, baada ya kumalizika kwa mkutano wake na viongozi wa vilabu vya michezo nchini, mkutano huo ulifanyika katika Ofisi  Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na viongozi wa vilabu vya michezo nchini kupitia Bodi ya Ligi, wakati alipokutana nao kuzungumzia maendeleo ya sekta ya mpira wa miguu pamoja na changamoto wanazopitia, kikao hicho kimefanyika Ofisi Ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi na Makamu wa Pili wa Rais Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) Bw. Steven Mnguto, akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba na viongozi wa vilabu vya michezo nchini, mkutano huo ulifanyika katika Ofisi  Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WFM- Dar es Salaam)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.