Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akikata utepe kwa ajili ya makabidhiano ya nyaraka za ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inayotarajiwa kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, CPA. Devotha Ngulugulu.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa mwakilishi wa TBA, Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Mwakilishi wa SUMA JKT, Jacob Gati (wa kwanza kushoto) wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa pili kulia) akishuhudia wawakilishi wa TBA wakiwaonesha mipaka wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. James Kibamba na kulia ni Mkurugenzi wa Mipango, Dkt. Abdul Mussa.
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tano kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja
na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya
SUMA JKT na TBA na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa
makabidhiano ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi Mji wa Serikali Mtumba,
Dodoma.
Na Prisca Ulomi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dodoma
Wawakilishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS)
wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende leo tarehe
18 Juni, 2022 wameshuhudia
makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu
wa Serikali lenye ukubwa wa mita za
mraba 17,342. Makabidhiano
hayo yamefanyika kwenye
Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma baina ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye
ni Mshauri Elekezi aliyewakilishwa na Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Kampuni ya
Ujenzi ya SUMA JKT ambae ni Mkandarasi iliyowakilishwa na Mkadiriaji Majenzi,
Jacob Ghati.
Akikabidhi eneo hilo, Mwakilishi wa TBA, Ng’olo ameeleza
kuwa jengo la Ofisi linalotarajiwa kujengwa ni la kisasa na ni miongoni mwa
majengo yenye muonekano mzuri katika Mji wa Serikali Mtumba. Jengo hili litakuwa na miundombinu
mbalimbali ikiwemo vyumba vya Ofisi 127, maegesho ya magari 111, maktaba, kumbi
2 za mikutano zenye nafasi 108 kila mmoja, kumbi 2 za kutolea mafunzo zenye
nafasi 42 kila mmoja, maabara ya kompyuta, vyumba vidogo 10 vya mikutano na chumba
cha akina mama wanyonyeshao. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika
kipindi cha miezi kumi na nane
(18).
Akizungumza kwa niaba ya Mkandarasi, Gati amesema kuwa
wako tayari kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa mkataba na kwa
kushirikiana na Mshauri Elekezi (TBA) na Mshitiri (OWMS).
Kwa upande wake, Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Dkt. Luhende amewatakia Mkandarasi na Mshauri Elekezi utekelezaji
mwema wa majukumu yao kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia weledi. Pia
amewahakikishia kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali itawapa ushirikiano
unaostahili.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment