Habari za Punde

Wakandarasi Watakiwa Kuongeza Kasi ya Ujenzi wa Mji wa Serikali.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu (katikati) akikagua jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za wizara 26  Awamu ya Pili katka Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu (kulia) akiwa na Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe (kushoto) wakikagua Maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais-Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala bora.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu  Dkt. John Jingu  (katikati) akikagua jengo la Wizara ya Katiba na Sheria katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi ya Ofisi za wizara zote, Awamu ya Pili katika Mji wa Serikali Mtumba.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu- Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amewataka wakandarasi wanaojenga majengo ya Wizara Awamu ya Pili katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma kuongeza kasi ya ujenzi   ili kumaliza kwa wakati.

Dk. Jingu alitoa  kauli hiyo  Jijini Dodoma  alipofanya ziara yake kutembelea na kukagua  maendeleo ya  ujenzi  huo ambapo alisema ujenzi unaendelea vizuri  huku  akiwahimiza kuongeza wafanyakazi.

Pia aliwaagiza kuongeza  muda wa kazi  na kuongeza vifaa  hatua itakayorahisisha kazi hiyo kufanyika kwa kasi inayotarajiwa  ili  ofisi hizo kuanza kutumika mara moja  akisema  kulingana na hali ya ujenzi baadhi ya majengo yatamalizika kabla ya muda uliopangwa.

“Kwa ujumla ni kwamba ujenzi unaenda vizuri  ushauri mkubwa ni tuongeze kasi ya utendaji  kazi na hasa kununua mahitaji ya vifaa kwa ujumla na wafanyakazi waongezwe itaweza kusaidia kwenda kwa kasi ambayo viongozi wetu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Waziri MKuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wanatarajia,” alisema Dkt. Jingu.

Aidha alieleza kwamba ni azima ya serikali kuhakikisha Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya Nchi linakuwa na miundo mbinu yenye ubora  na imara kama ilivyokuwa ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Nchi.

Naye Katibu wa Kikosi  Kazi cha Kuratibu  Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe alibainisha kuwa ujenzi unaoendelea ni wa wizara 26 na majengo 26  ukiwa umefikia hatua mbalimbali akisema umefikia asilimia 28 hadi asilimia 54.

“Kwa mfano ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala  Bora  umefikia asilimia 54, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  na Wizara ya Katiba na Sheria umefikia  wastani wa silimia 35 kazi hii inaenda vizuri na  inatarajiwa kumalizika katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni hadi Oktoba mwaka 2023 kwa ujenzi wa jumla  lakini baadhi ya majengo yatakamilika kuanzia Machi 2023,” alieleza Katibu  huyo.

Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi kutoka SUMA JKT Mhandisi Hagai Mziray aliahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu ya kuhakikisha wanaongeza vifaa na kasi ya ujenzi kufikia Aprili 2023 ujenzi uwe umekamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.