Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Ashiriki katika Hafla ya Chakula cha Hisani Cha EOTF.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika chakula cha hisani kilichoandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hasaan itaendeleza kukuza na kutoa ushirikiano kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikari (NGO) ili kuleta tija na maendeleo kwa jamii ya Watanzania.

 

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Juni 26, 2022) wakati wa hafla ya chakula cha hisani iliyoandaliwa na Shirika Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee  Jijini Dar es Salaam.

 

Waziri Mkuu alisema jitihada za pamoja kati ya Serikali na EOTF zinahitajika ili kuweza kuifikia jamii yote ya Tanzania kimaendeleo.

 

“Mafanikio hayawezi kupatikana bila ya kuungwa mkono, wadau wetu muhimu ni kama vile Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), wahisani kutoka sekta ya wafanyabiashara,  mashirika ya maendeleo ya kimataifa, watu binafsi na  madhehebu ya dini.”

 

Aliongeza kuwa ili kufanikisha maendeleo ya jamii ni lazima watu  wawezeshwe katika kuimarisha uwezo wao wa  kukabiliana na changamoto zinazowazunguka kwa kubuni mbinu  kuzitatua.

 

Waziri Mkuu  aliupongeza mfuko wa EOTF kwa kuendelea kutoa huduma kwa jamii ya Watanzania kwa kipindi cha miaka 25 sasa na kwamba huduma hiyo imeleta mabadiliko kwa wananchi katika nyanja za afya, elimu na uchumi.

 

“Wote tumesikia kuhusu historia na kazi zilizizofanywa na EOTF na mchango mkubwa wanaoutoa kwa jamii. EOFT wanastahili pongezi nyingi sana kwa jitihada kubwa wanazozifanya ambazo leo zimeifanya taasisi hii kuwa miongoni mwa taasisi imara ambazo zimekuwa zikizaa matunda. Nami nitumie fursa hii kwa moyo wa dhati kuwapongeza kwa mafanikio yote mliyoyapata katika kipindi chote cha miaka 25.”

 

Waziri Mkuu alimpongeza Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mama Anna Mkapa pamoja na wadau wengine kwa kusimamia vyema utendaji wa taasisi hiyo ambayo imetimiza malengo ya kuanzishwa kwake.

 

“Nimefurahishwa sana na programu zinazoendeshwa na taasisi hii hususan programu ya “Women Business Center “(WBC) mnayoanzisha ambayo itatoa huduma za masoko, elimu ya ujasiriamali, biashara, upatikanaji wa mitaji, afya ya mama na mtoto.”

  

Mheshimiwa Majaliwa alihitimisha kwa kusema kuwa Serikali itaendelea na jitihada mbalimbali za kuwakwamua wananchi kiuchumi kwa kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi na kutumia nyenzo za ndani kama mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum pamoja na TASAF ili kuzisaidia kaya masikini kujikwamua.

 

Kwa uapnde wake, Mwenyekiti wa EOTF, Mama Anna Mkapa alisema katika kuelekea awamu ya pili baada ya miaka 25, taasisi hiyo imeazimia kusonga mbele kidigitali kuwafikisha walengwa wake wanapostahili kijamii, kiuchumi, kiafya na kielimu kwa kuanzisha programu ya WBC.

Alisema program hiyo itatoa huduma za masoko, elimu ya ujasiriamali, biashara, upatikanaji wa mitaji, afya ya mama na mtoto na kufungua kituo cha kuweka bidhaa za wanawake wajasiriamali kutangaza bidhaa zao ndani na nje ya nchi. Kituo hiko kitatatua matatizo ya ajira, umaskini, ujinga na maradhi katika jamii yetu.

Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) Mama Anna Mkapa akizungumza katika chakula cha hisani  kilichoandaliwa na Mfuko huo kwenye ukumbi wa Diamond  Jubilee jijini Dar es salaam, Juni 26, 2022. Mgeni rasmi katika chakula hicho alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mama Mary Majaliwa  (kushoto)  wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa kwenye   chakula cha hisani kilichoandaliwa na mfuko huo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Juni 26, 2022. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.