Habari za Punde

KIWANDA CHA KUCHAKATA NYAMA NGURU HILLS KIMELETA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA UFUGAJI-PROF. NDALICHAKO


NA MWANDISHI WETU, MVOMERO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amesema kiwanda cha kuchakata  nyama cha Nguru Hills kinachomilikiwa na PSSSF na wabia wengine kimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya ufugaji.

Mhe. Profesa Ndalichako ameyasema hayo Julai 21, 2022 alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Shamba (Rachi) wa kunenepesha Mifugo na Machinjio ya kisasa wa Nguru Hills Ranch Wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro.

Alisema Mradi huo wa uwekezaji uliofanywa na PSSSF na wabia wenza, Kampuni ya Eclipse Investiment LLC na Kampuni ya Busara Investment LLP ni wa kupongezwa kwani licha ya kwamba kiwanda kiko kwenye majaribio tayari fursa zimneanza kufunguliwa kwa wafugaji na vijana.

“Kiwanda kina uwezo wa kuchinja Ng’ombe 100 na Mbuzi 1,500 kwa siku, soko kwa wafugaji litaongezeka.” Alisema

Alisema vijana pia watapata fursa kwa kupata kazi ya kunenepesha Ng’ombe kwa ajili ya kiwanda. “Kuna vikundi vitatu vya vijana vimepata mkopo kutoka Halmashauri, watafanya kazi ya unenepeshaji mifugo kwa kuandaa mashamba ya majani kwa ajili ya malisho ya mifugo.” Alifafanua.

Mhe. Profesa Ndalichako alionyesha matumaini yake kuwa Mradi utakapoanza kufanya kazi kwa ukamilifu utaongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo kama vile ngozi na nyama yenyewe.

“Ngozi zitakazopatikana kutoka kwenye kiwanda hiki zitakuwa na ubora wa hali ya juu kutokana na jinsi nilivyoona mchakato mzima wa uchinjaji.” Alisisitiza.

Alisema “Ni hatua nzuri na ninaamini Watanzania watanufaika hasahasa wafugaji kwenye mikoa ya Morogoro na mikoa jirani,”alisema

Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha uwekezaji wenye tija pia amefungua fursa nje ya nchi kwani masoko ya kuuza nyama nje tayari yamepatikana ya kutosha na hivyo bidhaa zitakazozalishwa kutoka kwenye kiwanda hicho licha ya kuuzwa kwenye soko la ndani pia zitasafirishwa nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, alisema Katika Mradi huo PSSSF inamiliki asilimia 39 ya hisa, huku wawekezaji wenza Kampuni ya Eclipse Investiment LLC kutoka Oman ikiwekeza hisa asilimia 46 na kampuni ya Busara Investment LLP ya hapa nchini imewekeza hisa asilimia 15.

“PSSSF imeweka kiasi cha shilingi bilioni 8.3 ambayo ni kama dola milioni 3.9 na tulikubaliana kwamba Mradi lazima ukidhi mahitaji ya Kimataifa.” Alifafanua.

Alisema Mradi una miundombinu inayohitajika kama vile eneo la malisho hekta 2,328 lenye uwezo wa kulisha Ng’ombe 10,000 na Mbuzi 15,000 kwa wakati mmoja.

Kuna jengo la utawala na jengo kubwa la kiwanda ikiwa ni pamoja na visima vitano vya maji vyenye uwezo wa kutoa lita elfu 20,000 kwa saa, pia tumejenga barabara za kuingia hapa ranchi ikiwa ni pamoja na mabwawa.

“Kwa sasa kiwanda kiko kwenye majaribio ya mwisho (testing and commissioning).” Alifafanua.

Alisema soko kuu la bidhaa hizo za nyama ni Mashariki ya Kati.

Mhe. Profesa Ndalichako akiangalia nyama kwenye kiwanda hicho.

 No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.