Habari za Punde

Mashindano ya ‘CRDB BANK NGALAWA RACE’ Yatajwa Kivutio cha Utalii Zanzibar

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma amesema mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi ni mfano wa       michezo ya utamaduni inayotangaza utalii visiwani humo.                                                                                     

Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akifungua mashindano katika hafla iliyofanyika kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni ambapo mamia ya watu walijitokeza kushudia mtanange mkali wa washiriki mahiri 20 wa mchezo wa ‘Resi za Ngalawa’ kutoka Kizimkazi Mkunguni na Kizimkazi Dimbani.

 

“Ni imani yangu ni kuwa mchezo huu utasaidia kuongeza thamani kwa fukwe zetu kwa kutoa burudani kwa watalii wanaotembelea katika visiwa vyetu, na kutoa ajira kwa vijana wetu,” amesema huku akitoa changamoto kwa Wizara za Michezo na Utalii kushirikiana na Benki hiyo kuendeleza mchezo huo.

 

Aidha, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kuwaletea wananchi maendeleo. “Niwapongeze kwa namna ambavyo mnajitoa kusaidia jamii. Ufadhili wenu katika miradi ya maendeleo hapa Kizimkazi unaonyesha kiu mliyonayo katika kuboresha maisha ya Watanzania.”

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa alisema Benki hiyo imeamua kuwekeza katika mchezo huo wa ‘Resi za Ngalawa’ kwa kuwa ni moja ya michezo ya asili hapa nchini ambayo ikitangazwa vizuri inaweza kutangaza utamaduni wa Wazanzibari na kuvutia watalii kuja kutembelea nchini.

 

“Rais wetu Mama Samia amefanya jitihada kubwa katika kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia filamu ya ‘Royal Tour’, tukiwa Benki kiongozi na ya kizalendo nchini tumeona ni vyema kuunga mkono jitihada hizi kupitia mashindano haya ambayo asili yake ni katika visiwa hivi vya Zanzibari,” amebainisha.

 

Akielezea lengo jengine la kuandaa mashindano hayo kwa mwaka wa pili mfululizo kupitia Tamasha la Kizimkazi, Tully alisema Benki ya CRDB pia imedhamiria kuutumia mchezo huo wa Resi za Ngalawa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuufanya mchezo kuwa wa kibiashara kama ilivyo michezo mingine.

 

“Katika kutekeleza azma hii, mwaka huu tumekabidhi vifaa vipya kwa washiriki wote 20 vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 50 ikiwamo ngalawa za kisasa na maboya ya uokoaji. Hii imeongeza hamasa kubwa sana kwa washiriki ambapo mashindano ya mwaka huu yamekuwa na ushindani mkubwa.”

 

Washiriki hao 20 walishindana katika resi za maili 2 kwa mizunguko miwili ambapo Khatib Haji Hamis mkaazi wa Kizimkazi Mkunguni aliibuka mshindi wa kwanza na kuondoka na zawadi ya shilingi milioni 2.5 na boti ya uvuvi kwa ajili ya kikundi kutoka kijiji anachotoka.

 

Mshindi wa pili alikuwa Juma Ramadhani Haji kutoka kijiji cha Kizimkazi Mkunguni ambaye aliondoka na kitita cha shilingi milioni 1, na watatu alikuwa Muhammad Ambar Mpate kutoka kijiji cha Kizimkazi Mkunguni ambaye aliibuka na zawadi ya shilingi laki 7, na mshindi wan ne alikuwa Daudi Wajihi Zahor mkazi wa Kizimkazi Dimbani ambaye alijishindia shilingi laki 5.

 

Mbali na mchezo wa wa “Resi za Ngalawa”, Benki ya CRDB pia imetumia zaidi ya shilingi milioni 65 kudhamini michezo mingine katika Tamasha la Kizimkazi ikiwamo; mpira wa miguu, mpira wa pete, nage, mbio za baiskeli, bao, kukuna nazi, kuvuta kamba, na uchoraji.

 

Aidha, Benki hiyo pia imejenga maabara ya kisasa ya sayansi iliyokamilika pamoja na vifaa vyake katika Skuli ya Kizimkazi yenye thamani ya shilingi milioni 50. Maabara hiyo inalenga kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sanyansi.

 

Tamasha la Kizimkazi linatarajiwa kufikia tamati siku ya jumamosi ya tarehe 3 Agosti 2022 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Miradi mbalimbali ya maendeleo inatarajiwa kukabidhiwa siku hiyo.

 

Kuhusu Benki ya CRDB

Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na wajasiriamali.

Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Benki ya CRDB ni Benki pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki iliyopata usaili wa Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (GCF).

Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara Tanzania na Burundi kwa kuhudumia wateja zaidi ya milioni 4 kupitia matawi 268, CRDB Wakala zaidi ya 22,000, ATMs zaidi ya 550, POS zaidi ya 1,800, na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.