Habari za Punde

Ujio Madaktari wa Kigeni Unaongeza Uwezo Kwa Madaktari Wazawa -Dk.Mwinyi.

 

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Korea National Turbaculosis Assosiation, inayoshuhulikia  Maradhi ya Kifua Kikuu (TB) Dr.Kyung Manho (kushoto) wakati wa mazungumza na Ujumbe huo leo walipofika Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Ujumbe wa madaktari kutoka Jumuiya ya Korea National Turbaculosis Assosiation, inayoshuhulikia  Maradhi ya Kifua Kikuu (TB), walipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo (wa tatu kulia) Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Dr.Kyung Manho

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ujio wa Madaktari  kutoka Jumuiya ya ‘Korea National Turbaculosis Association’ utafungua milango kwa Madaktari na Wataalamu  wa afya wa Taifa hilo kuja nchini kuwasaidia Wazanzibari katika kukabiliana na maradhi mbali mbali.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Timu ya Madaktari  15 kutoka Jumuiya ya Korea National Turbaculosis Association ya nchini ya Korea Kusini, waliokuja nchini kwa ajili kambi ya uchunguzi na matibabu ya Ugonjwa wa Turbaculosis (TB).

Amesema Zanzibar inakabiliwa na magonjwa mbali mbali, ikiwemo TB  na akabainisha mahitaji makubwa yaliopo katika upatikanaji wa madaktari na wataalamu wengine wa Afya ili kukabiliana na magonjwa hayo.

Alisema ujio wa madaktari hao utatoa fursa kwa Madaktari wazawa na wafanyakazi wa Afya kushirikiana na Madaktari wa Timu hiyo na kujenga uwezo  katika kakabiliana na ugonjwa huo, huku kukiwepo matarajio makubwa ya kuleta tija.

Aidha, alitoa shukrani kwa Madaktari hao kwa dhamira ya kuja nchini kuwasaidia Wazanzibari na kusema Zanzibar inatambua hatua kubwa iliofikiwa na Taifa la Korea Kusini katika kupambana na magonjwa mbali mbali, ikiwa na Madaktari na wataalamu wa Afya katika nyanja mbali mbali.

Mapema, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Korea National Turbaculosis Asssociationa Kyung  Manho alisema Jumuiya hiyo imefanya ziara  ya kuja Zanzibar ili   kujenga mashirikiano kati yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi ya TB.

Alisema hatua hiyo ni kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliipo kati ya Zanzibar na Taifa hilo la Korea Kusini.

Jumuiya ya Korea National Turbaculosis inayojishughulisha na kinga na matibabu  dhidi ya Ugonjwa wa TB, ilianzishwa mnamo mwaka 1953, ikiwa ni mara ya kwanza kufika hapa nchini, ambapo wakiwa nchini wataweka kambi na kutoa huduma za tiba kwa wagonjwa.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.