Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na wawekezaji
wa hewa ya ukaa kutoka Kampuni ya Carbon Exchange Market na Relevant Co.Ltd. pamoja
na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kikao cha kujadili
namna ya kushirikiana katika uwekezaji huo.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais.)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza misitu ili iweze kuleta fursa katika uwekezaji wa hewa ya ukaa.
Ametoa wito huo leo Agosti 15, 2022 alipokutana na wawekezaji
wa hewa ya ukaa pamoja na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais jijini
Dar es Salaam kujadili namna ya kushirikiana katika uwekezaji huo katika
kusaidia utunzaji wa mazingira.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wawekezaji hao wa
Kampuni ya Carbon Market Exchange kutoka Marekani na Relevant Co.Ltd. ya nchini
Tanzania, Waziri Jafo kupitia biashara ya hewa ya ukaa ana imani italeta
manufaa kwa mazingira na uchumi.
Alisema suala la ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa
limekuwa kubwa na kuwa takwimu zinaonesha takriban ekari laki nne zinapotea
hivyo hatuna budi kuendelea kupanda miti na kulinda misitu.
“Ni matarajio yetu kuwa kikao hiki kimefungua wigo wa
mjadala kuhusu namna gani biashara ya hewa ya ukaa inaweza kuwa na manufaa na
hata bajeti ya nchi yetu katika miaka inayokuja inawezekana tukawa na mapato
makubwa kutokana na biashara ya hewa ya ukaa,” alisema.
Aidha, Waziri Jafo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua za kukabiliana na athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia alisema kuwa miradi
ya Kimkakati ya Treni ya Umeme (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere
na Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (BRT) imekuwa ni miradi ya mfano kimataifa
katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Carbon
Market Exhange Bi. Shenna Forthers alisema wanatarajia kupata ushirikiano
kutoka Relevant Co.Ltd na Serikali ili kuweza kufanikisha azma ya utunzaji
mazingira.
Bi. Forhers aliongeza kuwa uwekezaji huo mbali ya
kutumia misitu pia unatarajiwa kuhusisha miti inayotokana na mazao ya korosho,
maparachichi na kahawa hivyo kuongeza wigo wa fursa.
Itakukumbukwa kuwa Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa
kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Glasgow nchini Scotland
miongoni mwa ajenda kuu ilikuwa ni namna ya nchi inaweza kufaidika na biashatra
ya hewa ya ukaa.
No comments:
Post a Comment