Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amefungua Msikiti wa Masjid Al Huda Masingini Wilaya ya Magharibi "A" Unguja

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kufungua Masjid Huda ulioko Masingini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja leo 23-9-2022,kabla ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo (kulia kwa Rais) Mkurugenzi Mkuu wa Al Noor Charitable Agency Zanzibar.Sheikh Nadir Mahfoudh na Sheikh Luay Mohammed Mahfoudh na (kushoto kwa Rais) Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar Sheikh.Khalid Ali Mfaume na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Alhaj Haroun Ali Suleiman

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Misikiti pamoja na Madrasa zinazojengwa zinapaswa kutumika kuielimisha jamii umuhimu wa malezi bora ya watoto ili wawe na khofu ya Mungu.

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo, katika  ufunguzi wa Msikiti mpya wa Al hudda  uliopo eneo la Masingini Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja,  uliojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya ‘Al-noor Cheritabla Agency for the Needy’, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema kumekuwepo mmong’onyoko mkubwa wa maadili katika jamii hususan kwa vijana kujihusisha na vitendo viovu, ikiwemo vya  Udhalilishaji, matumizi ya  dawa za kulevya pamoja na Wizi na ubadhirifu wa mali za Serikali, mambo aliyoeleza yanapaswa kuzungumzwa na kupatiwa ufumbuzi kupitia Misikiti.

Alisema matukio hayo na mengineyo mengi yalio kinyume na maadili yamekuwa yakifanyika kwa vile jamii imekosa khofu ya Mungu, hivyo akatoa rai kwa jamii kuimarisha malezi mema kwa watoto tangu wanagli wadogo ili waweze kukua wakiwa na khofu ya Mungu.

Katika hatua nyengine, Alhaj Dk. Mwinyi aliutaka uongozi kusimamia utunzaji wa msikiti huo  ili waumini wanaofika   waweze kutekeleza ibada  katika mazingira bora.

Aliwapongeza wafadhili waliojenga msikiti huo pamoja na wananchi wote waliofanikisha ujenzi huo na akatumia fursa hiyo kuwashukuru kwa dhati kwa kujenga eneo la kuchezea watoto, akibainisha hatua hiyo itatoa fursa kwao ya kucheza pamoja na kujifunza.

Aidha, aliipongeza taasisi ya Al –Noor Cheritable Agency for the Needy kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuenga majengo mbali mbali ya kidini pamoja na Huduma za kijamii katika ameneo mbali mbali nchini.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab alisema hatua ya Rais Alhaj Dk. Mwinyi ya kufungua msikiti huo ni kitendo kitukufu kilichopata kufanywa na Mtume Muhammad (SAW).

Mapema, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali mfaume aliwataka waislamu kuuimarisha msikiti huo kwa kuunadhifisha na kuufanyia matengenezo pale unapoharibika, sambamba na kutumika kama kituo cha kupata taaluma.

Sheikh Khalid aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kuwatupia lawama Viongozi kwa mambo maovu yanayofanyika katika jamii na akatumia fursa hiyo kuitaka jamii kufanya juhudi kuyaondoa maovu hayo kwa mikono yao.

Alisema katika zama hizi mitandao imekuwa ikitumika vibaya kubadili mitazamo ya mambo mema ili yaonekane mabaya na hayana manufaa yoyote kwa jamii, akitolea mfano suala la Utalii, ambapo ndani ya Kuraani limebainishwa kuwa na manufaa.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa ‘Al-noor Cheritable Agency for the Needy ‘ Sheikh Nadir Mahafoudh aliushukuru uongozi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) kwa kusaidia upatikanaji wa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo pamoja na ujenzi wa ukuta.

Alisema Taasisi hiyo imekubali ombi la  la wananchi na Uongozi wa kikosdi hicho cha KMKM  la kujenga Kiliniki katika eneo hilo, ili kuwandolea shida  ya matibabu inayowakabili.

Alisema msikiti huo una uwezo wa kuswaliwa na waumini 700 kwa wakati mmoja kupitia eneo la ndani na nje, huku wanafunzi wapatao 250 wataweza kuapta fursa ya kujifunza katika madrasa hiyo.

Aidha,  Khatibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Abdulkarim Said alissitiza umuhimu wa waislamu kufanya juhudi na kiujenga, kujikurubisha,  kuipenda na kujishughulisha na masula mbali mbali yanayohusu msiikiti, kw akigezo cha kupata fadhila kubw akutoka kwa Mwenyezi Mungu.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia Hutuba ya Sala ya Ijumaa ikisomwa na Sheikh Abdulkarim Said, iliyofanyika katika Masjid Huda Masingini baada ya kuufungua Msikiti huo leo 23-9-2022 na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Alhaj Haroun Ali Suleiman.. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislam Masingini Wilaya ya Magharibi “A”Unguja, baada ya kuufungua Msikiti huo na Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Huda leo 23-9-2022
WAUMINI wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Huda Masingini Wilaya ya Magharibi “A”Unguja leo 23-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Ufunguo wa Masjid Al- Huda Imamu Mkuu wa Msikiti huo Sheikh Ali Rashid Khamis, baada ya kumalizika Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti huo uliofunguliwa leo 23-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akishiriki kuitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Huda Masingini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja leo 23-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Masjid Huda Masingini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja leo 23-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Masjid Huda Masingini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja leo 23-9-2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.