Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizindua jengo la ukumbi wa mikutano la Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga katika ziara ya kikazi leo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Jane John na wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo na Taasisi ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Serikali imepokea Euro milioni 6 sawa na shilingi bilioni 13.2 kutoka Shirika la Ujerumani la GIZ kwa ajili ya mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori hasa kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) wakati
wa ziara ya kikazi katika Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu
Sekamaganga Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.
“Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kiasi
cha shilingi bilioni 13.2 ambazo zitatumika katika kufanya utafiti wa maeneo
yenye changamoto za wanyama wakali na waharibifu, kutoa elimu kwa jamii
zinazoishi pembezoni mwa hifadhi kuhusu uhifadhi na kukabiliana na wanyama
wakali na waharibifu” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema
mradi huo wa miaka mitatu una lengo la kutoa ujuzi kwa jamii kuhusu namna ya
kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu ambapo jamii hizo zitasambaza ujuzi
kwa jamii nyinginezo.
Aidha,
amesema mafunzo hayo pia yatatolewa kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji(VGS) ili
kuongeza nguvu ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Mhe.
Masanja amefafanua kuwa endapo jamii zikipata uelewa wa namna ya kuhifadhi na
kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hakutakuwa na chuki baina ya
binadamu na shughuli za uhifadhi.
Naye, Mkuu
wa Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Jane John
amesema kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo ya Askari wa Wanyamapori wa Vijiji,
Askari wa Misitu wa Vijiji, Askari wanaosimamia fukwe za jamii, kozi kwa
viongozi na wajumbe wa kamati za maliasili za vijiji, Astashahada ya Utalii na
Waongoza Watalii pamoja na mafunzo ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Jane John akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia)na watumishi wa Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga kilichofanyika leo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma. Kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori,Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael.
No comments:
Post a Comment