Habari za Punde

Taasisi ya Nuru Foundation ina kila sababu kuona inawasaidia kielimu kwa kutafuta njia za kupata ufadhili na kupata vifaa visaidizi

 

Mwenyekiti wa Nuru Foundation Mama Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib akimkabidhi Katibu wa Umoja wa Watu wenye Vichwa vikubwa na mgongo wazi ndugu Hussein Moh’d Saleh zawadi ya mchele lishe na pembas kwa ajili ya wagonjwa mbali mbali wanaofika kwenye  nyumba yao ya matumaini iliyopo Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja huo ndugu Omar Kaiza Omar
Mwenyekiti wa Nuru Foundation Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib akimbeba mtoto na Huldat Faki mwenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi alipowatembelea katika nyumba yao ya matumaini iliyopo Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B

Mwenyekiti wa Nuru Foundation  Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib akizungumza na wazazi na walezi wa watoto wenye Vichwa vikubwa na mgongo wazi alipowatembelea katika nyumba yao ya matumaini iliyopo Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B

Na Mwandishi wetu OMKR.

Mwenyekiti wa Nuru Foundation Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib amesema Jumuiya yao imeamua kujikita zaidi kumuangalia mtoto wa aina yeyote hasa yatima na anaeishi kwenye mazingira magumu

Ameeeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuwatembelea watoto wenye vichwa maji na mgongo wazi katika kituo chao cha nyumba ya matumaini iliyopo eneo la Mwanakwerekwe ndani ya Wilaya ya Magharibi B.

Mama Zainab amesema kumlea mtoto mwenye kichwa maji na mgongo wazi kunahitaji elimu kwa mzazi na walezi ili kufahamu namna ya kumlea hatimae nae mtoto akuwe katika mazingira mazuri yaliyo salama katika hali zote

Ameahidi kuwa taasisi ya Nuru Foundation ina kila sababu kuona inawasaidia kielimu kwa kutafuta njia za kupata ufadhili na kupata vifaa visaidizi pamoja na kumuandaa kisaikolojia mama au familia yenye mtoto mwenye ulemavu wa aina hii ili waweze kujikomboa na kujihudumia kiuchumi.

Aidha amesema kuwa Taasisi ya Nuru Foundation pia ina jukumu la kumuwezesha mwanamke ambae kwa kawaida ndie mlezi anaekuwa karibu sana na watoto hivyo taasisi hio itaanza rasmi kutoa mafunzo kwa akina mama wenye watoto wenye ulemavu na mazingira magumu ili waweze kuwa na mipango mizuri ya kujiinua kimaisha.

Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Nuru Foundation ameikumbusha jamii kuwa na utamaduni wa kubadili matumizi ya vyakula na kuzingatia ulaji vyakula vyenye afya ili kulinda afya ya mwili hasa kwa akina mama wanapokuwa wajawazito na

Pia amewakumbusha akina baba kuwa karibu na wake zao hasa wakati wa ujauzito pamoja na kusaidiana ulezi mama anapojifungua kwani mtoto ni mtoto ila mwenye ulemavu anahitaji uangalizi zaidi

Nae Katibu wa Umoja wa wenye vichwa maji na mgongo wazi ndugu Hussein Moh’d Saleh ameishukuru Taasisi ya Nuru Foundation kwa kuwa ni taasisi ya mwanzo kuwatembelea na kutoa msaada ambao kwa sasa wanauhitaji

Hussein amesema nyumba ya matumaini inahitaji ushirikiano mkubwa na Serikali, jamii na taasisi zisizo za kiserikali na wafanya biashara ili kuweza kutatua kwa pamoja changamoto zinazowakabili ikiwemo pempas, suala elimu, vifaa visaidizi, chakula, wataalamu na kuandika miradi

Nao akina mama na walezi wa watoto wenye vichwa maji na mgongo wazi wameelezea changamoto wanazozipata kutoka kwa wanajamii ikiwa ni pamoja na kudharauliwa na familia, majirani, watoto kupewa majina mabaya na kuachika kwa waume

“siku moja alikuja jirani yangu kuniangalia akaniuliza nimeambiwa umezaa mtoto mlemavu nikamwambia ndio lakini baada kumuona akaniambia huyo si mtoto ni jini niliumia sana sana”alisema mama huyo ambae hakutaka jina lake kutajwa

Kina mama hao wamesema bado jamii hawajaelewa kuhusu watoto wenye ulemavu wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi hivyo wameomba jamii wapatiwe elimu ili kuondosha unyanyapaa na dharau.

Kikao pia kilihudhuriwa na Katibu wa Umoja huo Omar Kaiza Omar ambapo Mama Zainab amekubali kuwa mlezi wa umoja huo na kukabidhi zawadi ya Box 20 za mchele lishe na Pempas kwa ajili ya wale wanaofika katika nyumba yao mara wanapotoka hospitali baada ya kupata matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja na wale wanaosubiri matibabu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.