Menu

Wednesday, October 5, 2022

Kuna Umuhimu Mkubwa wa Kudumisha Dhamira ya Kweli katika Kutafuta Maelewano ya Kisiasa na Kijamii Hapa Nchini, ili Kujenga Mustakbali Mwema wa Taifa.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano wa Wadau wa Kujadili Masuala Mahsusi ya Zanzibar Yanayohusu Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kudumisha dhamira ya kweli katika kutafuta maelewano ya kisiasa na kijamii hapa nchini, ili kujenga mustakbali mwema wa Taifa.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Kujadili masuala mahsusi ya Zanzibar yanayohusu Dsemokrasia ya Vyama vya Siasa, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport Zanzibar.

Amesema Zanzibar haiwezi kufikia maelewano ya kweli ya kisiasa, ikiwa jamii badala ya kushirikiana kurekebisha kasoro zinazojitokeza, baadhi ya watu wanatafuta visingizo vya kulaumiana.

Alisema ili kufikia hatua ya maelewano, kuna umuhimu mkubwa wa kuvumiliana, kustahamiliana pamoja na kusahau mambo mbali yaliopita.

“Maelewano ya kijamii hayawezi kudumu iwapo kila siku mtakuwa mnakumbushana au kutishana kwa mambo yaliopita”alisema.

Alieleza kuwa kiini cha maridhiano ni ujasiri na kuachana na mambo yaliopita na kusema maelewano hayawezi kudumu iwapo wahusika watakuwa hawaaminiani.

Aidha, alibainisha mambo mbali mbali ambayo jamii inapaswa kuyazingatia ili kufikia maelewano ya kweli, ikiwemo kukubaliana juu ya mgawanyo wa majukumu ya ndani ya maelewamo au maridhiano yaliofikiwa.

Alisema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache Barani Afrika iliyo na utulivu mkubwa wa kisiasa na yenye utamaduni wa kuvumiliana na hivyo akasisitiza haja ya kuendeleza utamaduni huo.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwataka Viongozi na wadau wa siasa  kutoruhusu Itikadi zao za kisiasa kudhoofisha udugu, umoja  na mshikamano uliopo, na kubainisha umuhimu wa  kukaa pamoja ili kufikia suluhisho la kuondokana na tofauti za kisiasa.

“Tukae na kuzungumza ili kuondoa tofauti zetu ili tubakike wamoja, tudumishe amani na utulivu ii kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii”, alisema.

Alisema Viongozi wa kisiasa pamoja na wadau wa siasa  wana wajibu wa kukubaliana na uwepo wa tofauti za kisiasa baina yao na kwamwe wasiruhusu hali hiyo kuwa chanzo cha kufarikiana na kuhasimiana.

Vile vile aliwataka wadau wa siasa kuondokana na utaratibu utakaowajengea mazingira wanasiasa  kubadilika na badala yake wawawekee mazingira bora ya kimaendeleo pamoja na kudumisha upendo na umoja wa kitaifa.

Katika hatua nyengine, aliwataka washiriki wa mkutano huo  kutumia hekima, busara na uzoefu wao katika kutoa, kuchangia na kutetea hoja zinazowasilishwa ili hatimae  waweze kupata mapendekezo na maazimio yalio bora.

Dk. Mwinyi alibainisha matarajio yake kuwa mjadala huo utatekelezwa na kuhakikisha nchi inafanya Siasa za kistaarabu ili kujenga misingi ya amani na utulivu.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru  wadau wote waliochangia kufanikisha mkutano huo, ikiwemo washirka wa  maendeleo wa UNDP, NDI, IRI pamoja na USAID .

Nae, Waziri wa Nchi (OMPR) Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia vyema fursa waliyoipata, akibainisha kuwa ni muhimu na adhimu, kwa kigezo kuwa  kuna baadhi nchi wanaihitaji na hawaipati.

Aidha, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi alisema mkutano huo umewahusisha washirki kutoka katika makundi mbali mbali, ikiwemo Viongozi wa Vyama 19 vya Siasa, Mawaziri, Makatibu wakuu, Asasi za Kiraia, watu mashuhuri, Viongozi wa Dini pamoja na wanasiasa.

Alisema katika mkutano huo jumla ya mada nne zitawasilishwa, ikiwemo ya Masuala mahsusi ya Zanzibar yanayohusus Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa Zanzibar.

Mapema, Mwenyekiti wa Vyama vya Siasa Juma Ali Khatibu alisema kufanyika kwa mkutano huo ni jambo kubwa lenye mnasaba na misingi ya Utawala Bora, huku akimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuasisi mkutano huo wa kihistoria.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuelezea mambo muhimu ya msingi wa kitaifa kwa kuweka mbele uzalendo.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment