Habari za Punde

UVCCM Iringa Vijijini : Iringa Sio Soko la Wafanyakazi wa Ndani

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa Elia Kidavile akitoa kiasi cha shilingi laki mbili kwaajili ya kukarabati sakafu za shule ya msingi Mlolo wakati wa mahafali ya 59 toka kuanzishwa kwa shule hiyo
Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa Elia Kidavile akitoa vyeti kwa wahitimu wa shule ya msingi Mlolo wakati wa mahafali ya 59 toka kuanzishwa kwa shule hiyo.

Na Fredy Mgunda, Iringa.

MWENYEKITI wa jumuiya ya vijana wa chama cha mapinduzi wilaya ya Iringa vijijini (UVCCM) Elia kidavile amewataka wanafunzi wanaohitimu darasa na saba kukata kwenda kufanya kazi za ndani pindi wanapohitimu elimu ya msingi.

Akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Mlolo,Elia kidavile alisema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la madalali kuwarubuni wanafunzi kwenda kufanya kazi za ndani pindi tu wanapomaliza elimu msingi jambo ambalo limekuwa likikatisha ndoto za watoto wengi.

Kidavile aliwataka wazazi kukataa kabisa jambo hilo ambalo halina afya kwa maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Iringa vijijini pamoja na Taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari hivyo hakuna haja ya wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kufanya kazi za ndani pindi wanapohitimu elimu ya msingi.

Kidavile alisema kuwa mzazi yoyote yule anakayekutwa amempeleka mtoto wake kufanya kazi za ndani basi sheria zitachukua mkondo wake na UVCCM wilaya ya Iringa vijijini haikubaliani kabisa na wazazi wanaowapeleka watoto kufanya kazi za ndani,hivyo wazazi wanatakiwa kuwapeleka sekondari mara baada ya matokeo kutoka.

Alisisitiza kwa jamii ya wananchi wa Kijiji cha Mlolo kutoa taarifa kwa viongozi wa Kijiji,kata,tarafa na wilaya iwapo kuna mzazi amempeleka mtoto wake kufanya kazi za ndani au mtoto ametoroka kwenda kufanya kazi za ndani ili sheria ichukue mkondo wake.

Aidha mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa vijijini Elia kidavile alichangia kiasi cha shilingi laki mbili kwa ajili ya kukarabati sakafu za shule ya msingi Mlolo ambao imeharibika ili kuwawezesha walimu kutoa elimu bora bila kuwa na hofu ya miundombini ya darasa.

Awali akizungumza mbele ya mgeni rasmi,mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mlolo Salum Mtewa  alisema kuwa shule hiyo inakabiriwa na changamoto za ukosefu wa kompyuta,photokopi mashine, upungufu wa madawati, upungufu wa walimu na upungufu wa vifaa vya michezo kwa wanafunzi.

Mwalimu Mtewa alisema kuwa anashukuru mchango alioutoa mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa vijijini Mheshimiwa Elia kidavile katika shule hiyo ya msingi Mlolo.

Alisema kuwa anaungana na mgeni rasmi kukemea kitendo cha wanafunzi kwenda kufanya kazi za ndani pindi wanapohitimu elimu ya msingi kuwa kunawapotezea ndoto za maisha yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.