Habari za Punde

Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur'aan Zanzibar yaelezea changamoto inazokabiliana nazo mbele ya Rais Dk Hussein Mwinyi

 


STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                                     09.11.2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hatua ya Serikali ya kuongeza ujenzi wa madarasa katika skuli za Msingi na Sekondari nchini, utawawezesha wanafunzi  kushiriki kikamilifu katika masomo ya Dini (madrasa).

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na  Viongozi wa Jumuiya kuhifadhisha Quraan Zanzibar, ulioongozwa na Sheikh Suleiman Omar.

Amesema ujenzi wa madarasa katika skuli mbali mbali za msingi na Sekondari  Unguja na Pemba, unalenga kupunguza mlundikano wa wanafunzi madarasani, hali inayosababisha   kuwepo mikondo miwili ya masomo (asubuhi na mchana).

Alieleza kuwa Serikali inatambua uwepo wa changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kukosa muda wa kuhudhuria masomo ya dini katika vyuo na madrasa,na kusema wakati ujenzi huo ukiendelea Serikali kupitia Wizara ya Elimu itaangalia namna ya kupunguza tatizo hilo, hususan kwa wanafunzi wasiohusika na utaratibu wa kuingia madarasani kwa mikondo miwili.

Alisema ili kupatikana ufanisi wa suala hilo, mashirkiano yanahitajika kati ya Serikali, Wazazi pamoja na wasimamizi wa madrasa na vyuo hivyo.

“Mimi naamini kwa nguvu tulizoweka katika kuongeza madarasa, hatua hiyo itapunguza utaratibu uliopo wa mikondo miwili ya masomo na kutoa fursa ya vijana kwenda madrasa”, alisema.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kuwapatia nafasi za masomo ya Chuo Kikuu wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufanikiwa kuhifadhi Juzuu 30 za Kuraan, kupitia fursa zinazopatikana kutoka kwa wafadhili mbali mbali, hususan wale wa nchi za Kiislamu.

Hata hivyo aliwashauri wanafunzi hao kuingia kwenye mchakato wa kupata fursa za masomo ya Chuo Kikuu kupitia Bodi ya mikopo, kwa kigezo kuwa hatua hiyo itapunguza idadi  ya wanafunzi wenye mahitaji.

Alhaj Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Jumuiya hiyo kuwasilisha hati na michoro ya majengo ya Markaz yanayokusudiwa kujengwa katika eneo la Chwaka, Mkoa Kusini Unguja, ili juhudi za kupata wafadhili ziweze kufanyika na kufanikisha ujnezi huo hatua kwa hatua.

Katika hatua nyengine, Alhaj Mwinyi alisema suala la ushiriki wa Jumuiya hiyo katika  mashindano ya kuhifadhi Kuraan mjini Dubai na kubeba Bendera ya Zanzibar lina changamoto za Kidiplomasia kama ilivyo kwa Shirikisho la Mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) na azma yake ya kupata unachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Alitoa rai ya kuwepo mashindano kati ya washiriki wa pande mbili za Muungano ili kumpata mshindi atakaeweza kuiwakilisha nchi (Tanzania) katika mashindano hayo.

Aidha, alisema ni vyema kwa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) pamoja na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar kukaa pamoja na kuona namna bora  ya kulishughulikia suala hilo ili kila nchi iweze kupata mwakilishi.

Hata hivyo, Alhaj Mwinyi alisema Serikali inapanga kuwaita kwa mazungumzao wadau wote wanaohusika na suala hilo, akiwemo Balozi wa UAE.

Mapema, Amiri wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Kuraan Zanzibar Amiri Suleiman Omar aliwasilisha ombi la Jumuiya hiyo kwa Rais Alhaj Mwinyi akimuomba kuangalia uwezekano ya wawakilishi wa Jumuiya kupata fursa ya kushiriki katika mashindano ya kuhifadhi Kuraan Mjini Dubai, baada ya kuwepo kwa  changamoto za kidiplomasia.

Aidha, Amiri huyo aliwasilisha ombi la kupata fursa za masomo ya Chuo Kikuu  vijana waliomaliza  kidato cha sita (Form VI) na ambao  wamemaliza kuhifadhi Juzuu 30 za Kuraan tukufu, sambamba na wale waliomaliza kidato cha nne (F.VI) na kuhitaji kupata elimu katika ngazi ya Diploma.

Vile vile Amiri Suleiman alimuomba Alhaj Mwinyi kusaidia kupata ufadhili utakaofanikisha  ujenzi wa Markazi ya Jumuiya hiyo katika eneo la Chwaka, ambapo wastani wa miaka 20 imepita tangu kupata eneo hilo na limebaki bila kuendelezwa .

Pia aliomba Serikali kuangalia namna ya kudhibiti muda wa masomo kwa wanafunzi wa skuli za msingi na Sekondari, ili waweze kuhudhuria katika masomo ya Dini, wakati ambapo hivi sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika masomo hayo ya skuli.

 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.