Habari za Punde

Mhe.Nchemba Awataka Wanamipango Kupanga Mipango Inayotekelezeka

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akizungumza wakati wa Kongamano la Wanamipango la mwaka 2022  jijini Dar es Salaam.

Na: Ramadhani Kissimba na Josephine Majura - WFM DAR ES SALAAM

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka Wanamipango nchini kuwa makini, katika kupanga mipango ambayo wataweza kuitekeleza, kuifuatilia na kuitolea taarifa sahihi. Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango katika ufunguzi wa kongamano la Wanamipango Jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru aliwataka Wanamipango hao kujikita zaidi katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali.

 

Bw. Mafuru amewataka wanamipango hao kuendelea kuishauri Serikali njia bora ya kusimamia kikamilifu mipango ya nchi  ili kufikia maendeleo au mafanikio ya uchumi wa kipato cha juu kinachokusudiwa ‘Nawasihi wote kwa umoja wenu kuwa na mchango na ushauri wenye lengo la kupanga na kusimamia kikamilifu mipango ya Nchi yetu. Uwezo wenu madhubuti utaisaidia Serikali na Nchi kwa ujumla kuwa na mipango imara na njia sahihi ya kufikia maendeleo au mafanikio ya uchumi wa kipato cha juu tunaoutamani’ alisema Bw. Mafuru

 

Aidha, alifafanua kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa Wanamipango, serikali ya awamu ya sita imeweka msukumo wa kipekee wa kuimarisha kada ya Wanamipango ili Taifa liweze kupanga mipango shirikishi inayotekelezeka kwa maendeleo ya watu wake si kwa kizazi cha sasa pekee bali na kizazi kijacho.

 

Awali akiongea wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Kamishina wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali Milanzi alisema wanamipango ndio wanaondaa, kusimamia,kutekeleza na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango ya nchi.

 

Bw. Milanzi alisema kongamano la wanamipango hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uwezo  na mada mbalimbali zitawasilishwa, kubwa zaidi kongamano hilo litatumika katika kujadili kuhusu Dira mpya ya maendeleo ya Taifa, ambapo Dira inayoisha 2025 ilikuwa na dhima ya kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati ambapo nchi ilifikia lengo hilo miaka mitano kabla ya Dira hiyo kuisha, hivyo kongamano hili litatumika kuyalinda mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya maendeleo 2025 kwa kuja na Dira mpya ambayo itakuwa na mafanikio kuliko Dira tuliyonayo saa.

 

Bw. Mafuru aliwakumbusha Wanamipango chini ya mlezi wa wanamipango nchini ambaye ni  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu jukumu lao la msingi la kusimamia kikamilifu ufuatiliaji wa Mipango ya nchi ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kama ilivyopangwa. ‘Labda niwakumbushe tu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kadhaa amesema kuhusu UDHAIFU WA KUFUATILIA MIPANGO YETU, suala hili kimsingi linaangukia kwenu Wanamipango. Nawaasa, chini ya Mlezi wenu kuwa makini katika kupanga mipango ambayo mtaweza kuitekeleza, kuifuatilia na kuitolea taarifa pasina shaka yoyote’ aliongeza Bw. Mafuru.

 

Aidha, Bw. Mafuru alisema kuwa kongamano hilo limekuja katika muda muafaka ambapo maandalizi ya awali ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 (TDV 2050) yameanza kutokana na nchi kuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2020/21 - 2025/26., hivyo kuwataka wanamipango kutumia kongamano hilo kuwa sehemu ya maandalizi ya Dira shirikishi ambayo itajumuisha maoni ya wadau wote muhimu.


Kongamano la mwaka la wanamipango linafanyika kwa siku tatu kuanzia                    tarehe 5 Desemba, 2022 lilobeba dhima ya ‘Mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa kizazi kijacho’ na limeshirikisha wachumi, wanamipango na watakwimu kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Fursali Milanzi akizungumza wakati wa Kongamano la Wanamipango la mwaka 2022  jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wanamipango wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (hayupo pichani), wakati wa Kongamano la Wanamipango la mwaka 2022  jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati) na Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Fursali Milanzi (wa pili kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti ya maandalizi ya Kongamano la Wanamipango la mwaka 2022  linalofanyika jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Daima Associations Prof. Samuel Wangwe, Kamishna Msaidizi  wa  Idara ya Mipango Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Royal Lyanga, wa kwanza kulia ni Mwakilishi Mkazi Msaidizi wa UNDP Bw. Amon   Manyama.

 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -WFM)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.