Habari za Punde

Wenye ulemavu walilia Mpango wa serikali kumaliza vitendo vya ukatili umepitwa na wakati

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 

ZANZIBAR 
Watu wenye ulemavu wametoa kilio chao juu ya  kupitwa na wakati pamoja na kutoingizwa masuala ya watu wenye ulemavu katika Mpango wa Serikali wa Kitaifa wa kumaliza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto NPA wa mwaka 2017-2022.

Wakitoa michango yao kwa nyakati tofauti wakati wa Mkutano maalumu wa  kuelezea Mpango huo kwa watu wenye ulemavu, katika ukumbi wa UNFPA kinazini Mjini Unguja wamesema, kwa misingi ya mahitaji ya  watu wenye ulemavu mpango huu haukufikia malengo kutokana na kutoingizwa masuala yanayowahusu watu wenye ulemavu na badala yake kuingizwa zaidi masuala ya wanawake na watoto. 

Wamesema katika mpango huo wa NPA 2017-2022,  takwimu za matukio ya udhalilishaji haziwasemei watu wenye ulemavu na badala yake zinawasemea wanawake na watoto tu,  pamoja na kutozingatia utekelezaji wa ahadi za nchi kwa watu wenye ulemavu.

Hivyo watu wenye ulemavu wamekubaliana  (NPA) hiyo iandaliwe upya na kuomba kuoainishwa takwimu za watu wenye ulemavu huku wakisisitoza nyenzo zitumike katika kuonesha mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Pia wameomba bajeti  iongezwe kwa ajili ya mahitaji ya watu wenye ulemavu pamoja na kuangaliwa kwa ukaribu zaidi takwimu za ajira kwani  haziendani na hali halisi ya mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Hata hivyo wamesema wanapoandika NPA mpya ni vyema pia kuzingatia  madrasa kwani muda mwingi watoto wanasoma madrasa na huko pia  kunafanyika vitendo vya udhalilishaji.

Mapema akiwasilisha maada ya Hali ya watu wenye ulemavu katika mpango wa Taifa wa Kumaliza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto(NPA) ya 2017-2022,  Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA Dk Masoud Hemed Nassor amesema mpango huo umeweka mkazo maalumu wa kumaliza vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.

Hata hivyo amesema kuwa lengo ni kuwaelezea watu wenye ulemavu mpango huo ili  waweze kuufahamu kwa undani pamoja na kutoa maoni yao wanapohisi uhitaji wa watu wenye ulemavu unapaswa kuingizwa katika mpango huo wa Taifa.

Pia Dk Masoud amesema mkutano huo umetoa nafasi  kuona mafanikio na changamoto katika mpango huo na kutoa kipaombele nini kifanyike katika kuwasaidia watu wenye ulemavu katika mpango huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.