Habari za Punde

Kufunguliwa kwa Diko na Soko la Samaki la Kisasa Malindi ni Ushuhuda wa Vitendo kwa Wazanzibari Kuutafsiri Maana Halisi ya Uchumi wa Buluu Visiwani

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kukamilika kwa diko la kisasa na soko la Samaki Malindi ni ushuhuda wa vitendo kwa Wazanzibari kuutafsiri maana halisi ya Uchumi wa Buluu, visiwani.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofungua diko hilo ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Uchumi wa Buluu unakamilishwa na mambo matano muhimu ukiwemo Utalii ambao kwa visiwa vya Unguja na Pemba una vivutio vizuri vinavyoingiza wageni kila uchao, uvuvi wa mwani na bahari alisema ni uchumi unaoendelea kufanywa wa wananchi wa visiwa wiwili hivyo, mafuta na gesi pamoja na usafirishaji wa majini na maeneo ya bahari ambayo hutoa fursa nyingi za kiuchumi kwa wakaazi wa maeneo hayo.

Alisema wakati Uchumi wa Buluu unagusa zaidi sekta ya uvuvi, alisema kuna haja ya wavuvi kutumia vyombo vya kisasa vya kuvulia zikiwemo zana za utambuzi wa samaki kwenye bahari, zana za GPS ambazo zitaongeza weledi wavuvi, kuvua kiwango kikubwa cha samaki wenye ubora.

Nakuongeza kujengwa vyumba vya kuhifadhia baridi kwaajili ya kuwekea samaki muda mrefu, mitambo ya kutengeneza barafu pamoja na viwanda vya kuchakata samaki kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi pamoja na kuwa na babdari ya uvuvi ni mambo yakuzingaliwa kwenye sekta hiyo.

“Tumeanza kuwawezesha wavuvi wetu kwa vyombo vidogovidogo, nataka tufike katika vile vyombo vikubwa ili wavuvi wetu waje na samaki wakubwa zaidi” Alieleza Dk. Mwinyi

Aidha, alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane itawazezesha wavuvi kufikia adhma ya Uchumi wa Buluu kwa vitendo na kuongeza kuwa serikali inakusudia kujenga madiko na masoko ya kisasa ya samaki kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Rais Mwinyi alisema serikali pia itashirikiana na sekta binafi kuimashirisha mafanikio ya soko hilo na kufahamisha serikali pekee haitoshi kukalisha kila kitu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamo wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alisisitisha suala la usafi na kuziagiza mamlaka husika za diko hilo kusimamia vyema kutunza haiba na mandhari ya eneo hilo.

Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Suleiman Masoud Makame alisema Wizara yake itashirikiana na serikali ya Mkoa wa mjini Magharibi kuhakisha diko na soko hilo yanaendelea kudumu na aubora wake

Mapema alikizungumza kwenye hadhara hilyo, Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Yamamura Naofumi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Mshirika mzuri na shirika hilo wamekua bega kwa bega kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo  maji safi, umeme, barabara, afya  na elimu.

Kwa upande wake Balozi wa Japani nchini, Yasushi Misawa aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kuipa ushirikiano wa kila hali na kueleza kwamba yeye ni muumini mzuri wa masoko ya samaki hivyo, aliwasihi wasimamizi wa diko hilo kuendelea kulitunza ili liishi muda mrefu, aidha, alieleza Tanzania na Japan ni washirika wa muda mrefu na kwamba uhusiano wa pande mbili hizo umejenga historia kubwa baina yao

Diko la Soko la samaki la Malindi limejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) linajumuisha ujenzi wa bandari na diko la maegesho ya boti, jengo jipya la soko na ofisi zake, miungombinu ya kuhifadhia samaki, mtambo wa kuzalisha barafu pamoja na ukarabati wa soko la zamani.

Aidha, dilo hilo linatarajia kuhudumia watumiaji 6500 wakiwemo wavuvi, madalali, wachuuzi, wauzaji rejareja, washushaji wa samaki, wasarifu samaki, walaji na wanachi wengine. Pia lina maeneo sita ya kuendeshea mnada, meza 141 za wauzaji wadogo wadogo zikiwemo baraza 76 na meza za kuhamishia 65, sehemu 13 za kuparia samaki, ujenzi wa diko la maegesho ya vyombo vidogo vipatavyo 392 kwa siku moja, vyoo 14, sehemu 6 za kuogea, vyumba vya kuhifadhia samaki wa tani 200 kwa wakati mmoja pia diko hilo linatarajia kutoa ajira 1400 kwaajili ya kushusha na kuhifadhi samaki.

IDARA YAMAWASILIANO,

IKULU

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.