RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza
taasisi binafsi kwa juhudi zao za kuiungamkono Serikali katika kuimarisha
huduma za jamii nchini.
Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo, Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es
Salaam, alipofungua kituo cha
kisasa cha afya cha Kairuki Green IVF cha hospitali ya Kairuki.
Alisema
dhamira za Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania ni kuimarisha huduma za afya ili kufikia hatua ya kuanzaisha Utalii wa
tiba kwa watu kutoka mataifa mengine kuja kufuata huduma za tiba, Tanzania.
Alieleza
uwekezaji mkubwa unaofanywa na taasisi binafsi na Serikali wa kuimarisha huduma
za afya nchini, dhamira hiyo inaanza kuonekana kwa sekta zote mbili za umma na
binafsi.
Alisema hospitali
ya Kairuki imekuwa tegemeo kwa Tanzania kutokana na huduma bora za afya
wanazozitoa kwa wananchi zikiwemo huduma za matibabu bingwa pamoja na vipimo
vya kisasa vyenye teknolojia ya hali ya juu.
Alieleza hospitali
hiyo imekuwa ya kwanza Tanzania kutoa huduma kadhaa ambazo awali hazikupatikana
kwenye hospitali nyengine zikiwemo vipimo vya “CT Scanner” vilipoanza
kutolewa na hospitali hiyo tokea mwaka 1992, huduma za upasuaji kwa kutumia
teknolojia ya kisasa ya “Laparascopy” ambayo ilianza kutolewa
hospitalini hapo mwaka 1996 pamoja na uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha kwanza
nchini cha binafsi cha Tiba
Alisema Chuo
kimetoa mchango mkubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa fani mbali mbali
za afya ambao sasa wanatumikia nchini na mataifa mbalimbali ya Afrika na
kwengineko duniani.
“Leo tena
tunashuhudia ufunguzi wa kituo cha kisasa kabisa cha Kairuki Green IVF ambacho
ni mafanikio makubwa na mapinduzi katika kuboresha utoaji wa huduma za afya
hapa Tanzania, Nakupongezeni sana” Dk. Mwinyi aliipongeza taasisi hiyo.
Aidha,
aliwahakikishia taasisi hiyo kwamba Serikali zote mbili zitakuza ushirikiano
nao kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa Watanzania na kuyafikia malengo
ya Kitaifa na Kimataifa kuboresha sekta ya afya nchini.
Dk. Mwinyi
alisema huduma za afya zinazotolewa na hospitali ya Kairuki zinakwenda sambamba
na Programu za Wizara ya Afya zikiwemo afya ya uzazi na watoto, mapambano dhidi
ya UKIMWI, Kifua kikuu, Malaria na UVIKO – 19.
Alieleza huduma
hizo ni mfano bora wa ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi. Aidha, alitoa wito
kwa taasisi binafsi kuendeleza ushirikiano wao na Serikali katika kuwatumikia
Watanzania.
Hata hivyo
Dk. Mwinyi aliitaka Wizara ya Afya Zanzibar kuona haja ya kuimarisha
ushirikiano baina yao na taasisi hiyo kwa kuzingatia uzoefu mkubwa walionao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mtendaji Mkuu
wa kituo cha Green IVF, Dk. Clementina Kairuki alisema, kituo kimeanzishwa kwa
lengo la kutoa huduma ya kupandikiza mimba kwa wanawake na wanandoa
walioshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida.
Alisema
uanzishwaji wa huduma hizo ni mwendelezo wa maono ya Muasisi wa taasisis hiyo
ya afya na elimu ya Kairuki, hayati Prof. Hubert Kairuki aliefariki miaka 24
iliyopita ambaye alitamani kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya
Tanzania.
Kituo cha
afya cha Kairuki Green IVF, kinatoa huduma ya kupandikiza mimba kwa
wanaoshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, kinamilikiwa na taasisi ya
afya na elimu ya Kairuki “(Kairuki Health and Education Network - KHEN),
kinasimamiwa na hospitali ya Kairuki, Kituo kipo Bunju ‘A’ Mianzini, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam.
IDARA YA MAWASILIANO
- IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment