Habari za Punde

RC.Senyamule Awakaribisha Mabalozi Dodoma

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe. Tri Yogo Jatmiko katika Ofisi yake iliyopo jengo la Mkapa, Jijini Dodoma. Mazungumzo yao yamelenga kuimarisha ushirikiano baina ya Jiji la Dodoma na Majiji ya Indonesia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akisalimiana na Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe. Tri Yogo Jatmiko katika Ofisi yake iliyopo jengo la Mkapa, Jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Senyamule na Katibu Tawala Mkoa Dkt. Fatuma Mganga wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo baina yao na ujumbe ulioongozana na Balozi wa Indonesia Tri Yogo Jatmiko.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini  Mhe. Yasushi Misawa (Wa pili kulia) na Katibu Tawala Mkoa na ujumbe wa wageni kutoka Japan wakiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Japan walipotembelewa na ugeni kutoka Ubalozi wa Japan nchini Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo tarehe 15/03/2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan Mhe.Yasushi Misawa na Mhe. Tri Yogo Jatmiko balozi wa Indonesia nchini Tanzania, katika Ofisi yake Dodoma.

 

Kwa nyakati tofauti Balozi wa Japan Mhe.Yasushi Misawa ameonesha nia ya kuhamia katika Jiji la Dodoma kuendeleza juhudi ya Serikali katika kuhakikisha balozi na mashirika ya kimataifa yanahamia Dodoma Makao Makuu ya nchi.

 

Balozi Misawa amesema pia ujio wa Ubalozi wa Japan katika makao makuu ya nchi una lengo la kuimarisha ushirikiano uliopo wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili ikiwa ni pamoja na kuona maeneo mahsusi ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda.

 

Kwa upande mwingine, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Tri Yogo Jatmiko amesema ujio wake umelenga kuanzisha ushirikiano baina Jiji la Dodoma na Jiji la Jakarta.

 

Amesema Indonesia iko tayari kushirikiana na Jiji la Dodoma katika kuendelea maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kukamua mafuta kupitia miti ya "Miarobaini"

 

Balozi Tri Yogo Jatmiko amesema nchi yake kwa upande wa Zanzibar inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwawezesha akina mama katika miradi ya kukamua mafuta ya karafuu.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya maboresho makubwa katika Mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na huduma za afya.

 

“Tunawakaribisha Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu, Fahari ya watanzania, Serikali imeimarisha kila sekta na baadhi ya Balozi na mashirika ya kimataifa yamehamia,nitoe shime kwao kufungua ofisi hapa na kuendelea kushirikiana nasi katika masuala ya maendeleo ya nchi yetu” Senyamule alisisiza.

 

Jumla ya viwanja 67 vimetengwa katika mji wa Serikali Mtumba kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Serikali na mashirika ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.