Habari za Punde

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (kushoto) akiwa na Balozi wa Marekani-Tanzania, Mhe. Michael Battle, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Dar es Salaam, ambapo Marekani imeahidi kuendelea kusaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa kasi zaidi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wapili kushoto) akizungumza na ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani ukiongozwa na Balozi wa Marekani-Tanzania, Mhe. Michael Battle, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Dar es Salaam, ambapo Marekani imeahidi kuendelea kusaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa kasi zaidi.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani-Tanzania, Mhe. Michael Battle (wa tatu kulia), alipofika kujitambulisha Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam. Wengine katika Picha ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID Bi.Kate Somvongsiri (wapili kulia), Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Rished Bade, anayefuata ni Afisa Biashara Mwandamizi wa Marekani nchini Bw. Ken Walsh (wa pili kushoto), na Afisa Itifaki wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Geitan Kobelo.

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

MAREKANI imeahidi kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha uchumi wake na maendeleo ya wananchi kwa kutoa fedha na ujuzi mbalimbali pamoja na kuvutia uwekezaji kupitia ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi. 

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam, alipofika kujitambulisha.

Mhe. Battle amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia na kukuza uchumi wa nchi na kuamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika Bajeti yake kwenye sekta za uzalishaji zinazogusa maisha ya watu, kikiwemo kilimo.

“Tunaahidi kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Kiongozi shupavu ambaye situ kwamba anapigania sana maisha ya watanzania, lakini pia amekuwa mwanadiplomasia anayepigania maendeleo na utangamano wa Afrika” alisema Mhe. Battle.

Mhe. Battle alisema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amegusa mioyo ya wamarekani na viongozi wake ndiyo sababu za Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamara Harris kupanga ziara ya kuitembelea Tanzania ambapo viongozi hao wawili watafungua fursa zaidi za ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliahidi kufikisha ujumbe wa Balozi huyo kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumwahidi kiongozi huyo kwamba Tanzania iko tayari kutumia fursa za ushirikiano wa nchi hizo mbili kuwahudumia Watanzania.

Aliiomba Marekani kupitia Shirika lake na Maendeleo la Kimataifa (USAID), kuhakikisha kuwa inazipa kipaumbele Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI) katika utekelezaji wa program zake mbalimbali hapa nchini kwa kuzijengea uwezo wa kifedha na kiuendeshaji badala ya kufadhili Taasisi za nje pekee zinazopewa fedha kutekeleza miradi hiyo badala ya kuzinufaisha AZAKI za hapa nchni.

Kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuzipa kipaumbele sekta za uzalishaji katika mgao wa fedha za Bajeti, Dkt. Nchemba alisema kuwa sekta hizo ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, uendelezaji wa wafanyabiashara wadogo (Machinga), utakuza uzalishaji wa mazao, lakini pia kuongeza ajira kwa wananchi hususan vijana.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) Bi. Kate Somvongsiri, alimshukuru Dkt. Nchemba kwa kutoa hoja ya Taasisi za wazawa zikiwemo AZAKI, kupewa kipaumbele katika miradi inayotekelezwa kupitia Shirika lake hapa nchini.

Alisema kuwa utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba asilimia 25 ya rasilimali zinazotumika na Shirika lake katika nchi zinaelekezwa kwenye taasisi za wazawa na kwamba kiwango hicho kitaendelea kuongezeka wakati unapowadia kufanya hivyo lakini lengo ni kufika asilimia 50.

Ushirikiano wa Tanzania na Marekani umetimiza zaidi ya miaka 50 ambapo makubaliano ya kwanza ya kuanzishwa kwa uhusiano huo yalisainiwa mwaka 1968.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.