Habari za Punde

Jamii Yahimizwa Kufanya Mazoezi kwa Afya Bora

Daktari dhamana wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja Bi.Maryam Hamdu Khalfan akizungumza na Wananchi wa kikundi cha  maradhi yasioambukiza alipokuwa akiwapatia elimu ya maradhi hayo wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za Afya katika ngazi ya jamii huko Bumbwini Makoba Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Afisa mradi wa kuwafikia wagonjwa wa maradhi yasioambukiza kutoka PharmAccess International Queen – Ruth Msina akimsaidia mzee kuingia katika chumba cha daktari wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za Afya katika ngazi ya jamii  kwa wagonjwa wa maradhi hayo huko  Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini “B”Unguja.
Picha na Fauzi Mussa –MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa Maelezo

Jamii imeshauriwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo kila siku ili kuondoa   takataka   zisizohitajika ambazo zinasababisha maradhi mbalimbali mwilini.

Daktari dhamana Wilaya ya Kaskazini "B" Maryam Hamdu Khalfan ameyasema hayo alipokuwa akitoa elimu ya Afya juu ya  maradhi yasioambukiza kwa wanakikundi cha  wagonjwa wa maradhi hayo  wakati wakipatiwa huduma za Afya katika ngazi ya jamii huko Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini "B"

Alifahamisha kuwa kutokufanya mazoezi kunapelekea mafuta kukaa na kuganda kwenye mishipa ya damu jambo ambalo linaifanya  mishipa hiyo Kuwa dhaifu na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi hivyo ameishauri jamii kufanya mazowezi angalau nusu saa kwa siku ili kusaidia  kuyeyusha mafuta hayo.

Aidha alifahamisha kuwa endapo mafuta yataganda katika mishipa ya damu kunasababisha maradhi ya sindikizo la juu la damu (presha) na hatimae kupelekea mtu kupata kiaharusi (stroke) maradhi ambayo yanapelekea ulemavu wa daima .

Alielezea kuwa kufanya mazoezi  mara kwa mara licha ya kuuchangamsha mwili na  kuuweka katika hali ya uimara pia  ni  njia moja wapo ya kujikinga na  maradhi hayo hivyo amesisitiza jamii kutokuwacha kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao.

"Jamii haina Utamaduni wa kufanya mazoezi tukidhani mazoezi ni kukimbia au  kubeba vyuma kumbe hata kutembea kwa   dakika 30 tu kunatosha   kuwa wewe umefanya mazoezi " Alisema Dkt. Maryam

Aidha Dkt.Maryam aliitaka jamii kupendelea kunywa maji ya moto ya limau kabla ya kula chochote  kwani kinywaji hicho kinarahisisha mzunguko wa damu na  kuyeyusha mafuta  mwilini.

"Unywaji wa  maji Moto yaliyochanganywa na kipande cha limau kunasaidia mzunguko wa damu na kufanya jasho litoke kwa wingi  mwilini, tujenge mazowea ya  kutumia maji haya ili tusafishe miili yetu kwa kutoa jasho jingi na kuisaidia mishipa ya damu kufanya zake yake." Dkt. Maryam alishauri

Hata hivyo dkt. Maryam aliwashauri  wanakikundi hao kushirikiana na wahaudumu wa afya wa kujitolea katika jamii (CHV)  kuandaa utaratibu maalum wa kukutana  na kufanya  mazowezi ili kupunguza msongo wa mawazo unaohatarisha afya zao.

Nae Daktari dhamana kituo cha Afya Bumbwini Misufini Aisha Ali  amewaomba wanakikundi hao kuwa na mashirikiano mazuri na kufuatilia huduma hizo Kila ifikapo tarehe waliopangiwa  na kuwataka  kutoa taarifa za dharura kwa madaktari pindi wanaapofikwa na tatizo kabla ya  tarehe yao ya kliniki kufika.

Kwaupande wao wanakikundi hao wameishukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na PharmaAccess International kuwasogezea huduma za Afya karibu na jamii na kuahidi kuitumia vyema  fursa hiyo yenye lengo la kuboresha huduma za Afya Nchini.

Itakumbukwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein  Ali Mwinyi amekua akiwasisitiza  wananchi kufanya  mazoezi kila siku ikiiaminika  kuwa kunaboresha  Afya zao na kuwakinga na maradhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.