RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amechangia shilingi
milioni 10 kwaajili ya ujenzi wa maduka matano, yanayokusudiwa kutoa gharama za
uendeshaji wa msikiti mkuu wa Paje, Mkoa wa Kusini, Unguja.
Al hajj Dk. Mwinyi alitoa mchango huo alipofungua msikiti
huo na kuiasa jamii na waumini msikitini hapo, kujitoa kwa hali na mali kuchangia
ujenzi wa maduka hayo ili kukamilisha ujenzi.
Alisema ujenzi wa maduka hayo utachangia gharama za
uendeshaji wa misikiti huko endapo utahitaji matengenezo na ukarabati, gharama
za maji na umeme pamoja na gharama za kuwalipa masheikh na maimamu
watakaouendesha msikiti huo.
Aidha, Al hajj Dk. Mwinyi aliwanasihi waumini na viongozi
wa msikiti huo kuutumia vyema kwa mambo ya khairati na yenye kujenga jamii
iliyobora, ikiwemo kusaliwa, kuwafundishia vijana maadili mema na kuwakataza
mabaya, ili kuwanusuru na majanga ya kilimwengu ikiwemo athari za dawa za
kilevya na masula ya udhalilishaji wa kijinsia.
Pia, aliwaeleza waumini hao lengo la kujengwa
misikiti hiyo kwa waumini ni kusaliwa kwa wakati na kufanyiwa ibada kwa wingi,
hivyo aliwaomba kujaza safu wakati wote wa kutekelezwa kwa ibada msikitini
hapo.
Al hajj Rais Dk. Mwinyi, pia alitumia fursa hiyo
kuwashukuru wafadhili wa ujenzi wa msikiti huo pamoja na kuwashukuru wazawa kwa
weledi wa kujitoa kwao kuanza ujenzi wa msikiti huo kabla ya kupata wafadhili.
“Tunawashukuru sana wafadhili wetu kwa kujitoa na
kuijenga misikiti mizuri na yenye hadhi kubwa kama huu, lakini ningependa zaidi
niwashukuru, niwapongeze na niwatakie kila la kheir wale ndugu zetu walioanza
ujenzi wa msikiti huu kabla ya kupata wafadhili, hawakukaa wakafunga mikono
wakasema tunamsubiri mfadhili, walianza wao. Hii ni imani kubwa walioionesha
kidogo walichokua nacho walianza nacho hadi walimaliza msingi wa jengo lote.”
Alipongeza Al hajj Dk. Mwinyi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema,
wananchi na waumini wa Mkoa wa Kusini Unguja wanaungamkono jitihada
zinazofanywa na Rais Al hajj Dk. Mwinyi.
Akizungumza kwenye halfa ya ufunguzi wa msikiti huo,
Mfadhili Dk. Maheer Bakari alieleza misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu, hivyo
aliwaomba waumini wazitukuze, wazitunze na kuziheshimu kwaajlili ya kimtaja
Mwenyezi Mungu muda nyakati zote.
Pia alimshukuru Rais Al Hajj Dk. Mwinyi kwa harakati
zake kwenye masuala ya dini.
Pia sheha wa Paje, Mohamed Rajab nae alieleza ujenzi
wa msikiti huo ulianza mwaka 2021 kwa wananchi wa shehia hiyo kujitolea
kuchimba msingi na kuutengeneza wote na mwaka jana walitokea wafadhali na
kuujenga msikiti huo hadi kukamilika kwake.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili hao kwa
kuukamilisha ujenzi wa msikiti huo.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment