Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ina wajibu wa kutenga
bajeti ya kuwawezesha watumishi wake hususan wa kada ya watunza kumbukumbu.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi
wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, (TRAMPA) uliofika
kujitambulisha.
Alisema bado Serikali
ina wajibu wa kuwapeleka masomoni na kuwaongezea uwezo watunza kumbukumbu na
watumishi wengine wa umma ili kuwajenga uweledi katika kukidhi haja ya taaluma
zao.
Alisema, chama cha
TRAMPA ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini ambacho kimejikita kwenye
weledi wa hali ya juu wa kuwainua wanachama wake kitaaluma na ufanisi.
Rais Dk. Mwinyi,
alitumia
fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu
Hassan kwa uamuzi wa kuuleta mkutano mkubwa wa chama cha TRAMPA kwenye visiwa
vya Zanzibar, nakueleza kuwa mbali na kufanikisha malengo ya mkutano huo, pia umeakisi
dhima ya utalii wa ndani.
Dk. Mwinyi alieleza
asilimia 30 ya uchumi wa Zanzibar unatokana na sekta ya Utalii, hivyo Mkutano
wa TRAMPA uliinufaisha sana Zanzibar kiuchumi na biashara hasa kwa sekta za umma,
binafsi na wananchi wakawaida.
Akizungumzia masuala
ya Utalii kwa wanachama hao wa TAMPA ambao walimzawadia Rais Dk. Mwinyi zawadi
ya sanamu ya mnyama wa Twiga ambae anasadifu utalii wa Wanyama uliopo nchini
kupitia rasilimali za misitu na mbuga za Wanyama ambavyo ni vivutio vikubwa kwa
wageni na watalii wanaofika nchini.
Dk. Mwinyi alieleza,
Zanzibar na Tanzania Bara kuna ushirikiano mkubwa katika kuitangaza na
kuishajihisha sekta ya utalii hususani wageni na watalii wanaobahatika kuitembelea
Tanzania, kwa pande zote mbili za Muungano hushajihishwa kutembelea vivutio vya
utalii kwa sehemu yoyote ile wanayofikia.
“Hapa Zanzibar tuna
jambo moja ambalo tunalitumia vizuri, kwamba wageni wanaotaka kwenda kwenye
mbuga, kule Tanzanaia Bara kwa uwindaji au iwe safari tu za kuangalia Wanyama,
aidha wanaanza kule lakini kisha lazima waje Zanzibar na wakianza huku lazima
waende Bara” Alifafanua Dk. Mwinyi.
Alieleza, Tanzania imeweka
utaratibu mzuri wa kuendelea kuutangaza utalii kwa nguvu zote, nakueleza kuwa kitu
ambacho kimeunganisha na kuendelea kuweka nguvu zaidi ili watalii wote wanaokuja
Tanzania japo kwa siku chache basi wapate nafasi ya kuja Zanzibar na wanaoanzia
Zanzibar pia waende Bara.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza faida za mkutano wa TRAMPA
visiwani hapa, kwamba uliwanufaisha wazawa wengi kuanzia wafanyabiashara wenye maduka,
vyakula, hoteli, nyumba za wageni hata sekta ya usafirishaji wakiwemo madereva taxi,
bodaboda, daladala na wafanyabiasahara wengine.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota George Mrope aliiomba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kutoa ushirikiano kwa kuwaruhusu watunza kumbukumbu wake
kuhudhurra mafunzo mbalimbali yatakayoandaliwa na chama hicho popote, ndani na
nje ya Zanzibar ili kuwaongezea weledi na uwezo wa kitaaluma watumishi hao.
Alieleza kufuatia Mkutano wa Chama cha Menejimenti ya Makatibu Mahsusi (TAPSEA) na Chama
cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika Mei 27 mwaka huu
maeneo ya Fumba, Zanzibar kuna baadhi ya wakuu wa taasisi za Umma walishindwa
kuwapa ruhusa watumishi wao ya kushiriki kwenye mkutano huo jambo aliloliomba kwa
Serikali kutoendelea tena ili kuwapa uwezo watumishi wao kushiriki kwenye mikutano
mkubwa kama hiyo kwani inawainua kifikra, weledi na kuwajengea ufanisi kwenye
taaluma zao.
Mrope alieleza
tukio la mkutano mkubwa wa Mei 27, limeandika historia mpya kwenye kumbukumba
ya kada yao pia wameuita ni ushindi kwao kwa kufanikiwa kukutana pamoja wana
taaluma wa kada ya watunza kumbukumbu zaidi ya 500.
Mwenyekiti huyo wa
TRAMPA alimueleza Dk. Mwinyi Chama chao hakisindikizi kwa Serikali wala
kujihusisha na shughuli zozote nje ya chama chao.
Aidha, wanachama
hao wa TRAMPA walitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dk. Mwinyi kuwa Mwanachama
wa chama hicho kwani mlezi wa chama hicho ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais
Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya pili.
Chama cha TRAMPA kilipata
usajili wake namba SA 19596, tokea 29 Agosti mwaka 2014 kutoka kwa msajili wa
vyama vya kijamii, Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, kilianzishwa kwa lengo la
kuwaunganisha wataalamu wa kumbukumbu na nyaraka Tanzania.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment