Habari za Punde

Taarifa ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar Yatolewa

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Masoud  Suleiman Makame akizungumza wakati alipokua Akitoa taarifa kwa  vyombo vya habari kuhusiana na  shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar,huko Ofisini kwake Maisara Mjini Unguja, Mei 11,2023.
Picha na Fauzia Mussa -Maelezo ZANZIBAR

Na Rahima Mohamed                                                              

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa juhudi mbalimbali zikiwemo kuhamisha data zilizochukuliwa katika maeneo ya Zanzibar kutoka Taasisi za Tanzania Bara ili kuendeleza shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.

Hayo yamesemwa  na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Masoud Suleiman Makame wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Maisara Mjini Zanzibar.

Amesema data hizo  ni  muhimu katika   utafutaji na uchimbaji  wa gesi asilia ambazo zimechukuliwa nyakati tofauti  katika eneo la bahari ya Mashariki mwa Zanzibar  na kitalu kinachoitwa Pemba Zanzibar Block.

Aidha amesema  Wizara ya Uchumi wa Buluu  kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia imesaini mkataba na Kampuni ya Kimataifa ya Schlumberger ili kuzitafsiri data hizo na kufanya tathmini ya maeneo yenye viashiria vya uwepo wa rasilimali hizo.

Vilevile amesema mkataba huo utawajengea uwezo watendaji wa Taasisi ya Mafuta na Gesi Asilia ,kukata vitalu vipya,pamoja na kuzitangaza data za Zanzibar katika majukwaa ya kitaifa ili kuweza kuwavutia wawekezaji wakubwa wa sekta ya mafuta na gesi asilia.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa shilingi milioni 700 za Kitanzania kwa ajili ya kuanza mchakato wa  ujenzi wa kituo cha Taifa cha Data za Mafuta Zanzibar ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.

Hata hivyo amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeanza na utaratibu wa kulifungua eneo la Pemba –Zanzibar kwa uwekezaji mpya wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta gesi asilia.

Waziri Masoud  amesema Serikali ikishirikiana na Kampuni ya RAKGAS inaendelea na zaoezi la ulipaji fidia wananchi walioathirika na zoezi hilo kwa njia ya mtetemo.

“Jumla ya madai 4,306 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.39 yalisajiliwa kwa Unguja na Pemba ambapo hadi sasa madai ya2,587 tayari yameshalipwa yenye thamani ya Bilioni 1.09 TZS”Alisema Waziri huyo.

Aidha amesema katika ulipaji wa fidia hizo changamoto mbalimbali zilijitokeza ikiwemo waliohakikiwa kurudia tena kudai,kutojaza fomu kikamilifu pamoja na wananchi kutoenda kufata fedha zao baada ya kukabidhiwa vocha za malipo.Hivyo aliwataka wananchi waliohakikiwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.